Apigia chapuo hifadhi ya mazingira, upatikanaji wa fedha na uhamishaji wa teknolojia
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Umoja wa Mataifa hauna budi kuyaunga mkono mataifa madogo ambayo hayana uwezo kiuchumi ili yaweze kuboresha mipango yao ya ndani.
Ameyasema hayo jana jioni (Jumapili, Septemba 22, 2024), wakati akiwasilisha salamu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye ufunguzi wa Mkutano wa siku mbili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kujadili Hatma ya Siku Zijazo (Summit of the Future) ulioanza jana kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani.
Waziri Mkuu ambaye yuko Marekani akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79), amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kuhusu jitihada za Serikali kwenye masuala ya uchumi, ulinzi na mabadiliko ya tabianchi.
Akifafanua kuhusu suala la uchumi, Waziri Mkuu amesema: “Umoja wa Mataifa tunauomba uyaunge mkono mataifa ambayo hayana uwezo ili yaweze kuboresha mipango yao kiuchumi waliyonayo ndani ya nchi yao. Tanzania tumepanga kujenga kesho iliyo bora kwa watu wetu kwa kuimarisha kilimo, uwekezaji, viwanda, madini na maliasili.”
“Unapozungumzia ujenzi wa kesho iliyo bora kwa watu wako, huwezi kufanikiwa kama hakuna nchi iliyo salama; kwa hiyo ulinzi na usalama ni suala la muhimu na tumeihakikishia jumuiya ya kimataifa kwamba pamoja na ulinzi wa ndani bado ulinzi kwa nchi jirani nao pia wa muhimu,” ameongeza.
Kuhusu suala la mabadiliko ya tabianchi, Waziri Mkuu amesema hivi sasa dunia inashuhudia athari kubwa kwenye baadhi ya nchi kutokana na shughuli za kijamii ikiwemo ukame, mvua nyingi zinazobababisha mafuriko. “Tanzania iko kwenye harakati za kuelimisha wananchi wake kuhusu mabadiliko ya tabia nchi ili waweze kukaa pamoja na kujadiliana namna ya kukabiliana nayo huku wakiendelea na kazi zao za kiuchumi,” amesisitiza.
Amewataka wajumbe wa mkutano huo wachukue hatua madhubuti za kupunguza uzalishaji wa hewa chafu, kulinda baioanwai na kuunga mkono jitihada za kukabiliana na hali hiyo katika nchi zinazoendelea. “Tanzania ina nia ya dhati ya kutetea masuala ya hali ya hewa duniani na inaitaka jumuiya ya kimataifa itimize ahadi zake za utoaji fedha za kusaidia masuala ya hali ya hewa na uhamishaji wa teknolojia.”
Mapema, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutierres alisema mkutano umeitishwa katika wakati huu ili waweze kutafuta mbinu za kuikomboa dunia kutoka huko inakoelekea na kuirejesha kwenye mstari wake. “Dunia imehama kwenye reli na sasa tunahitajika kufanya maamuzi magumu ili tuweze kuirejesha kwenye njia sahihi,” alisema.
“Niliitisha kikao hiki kwa sababu changamoto za karne ya 21 zinahitaji kutatuliwa na majibu ya karne ya 21 kwa kupitia mifumo ambayo imeundwa vema, iliyo jumuishi na inayohitaji utaalamu wa watu wote.”
Akianisha changamoto hizo, Katibu Mkuu huyo amezitaja baadhi kuwa ni kukithiri kwa migogoro kuanzia Mashariki ya Mbali hadi Ukraine na Sudan huku kukiwa hakuna matumaini ya kuisha; mifumo ya usalama inayotishiwa na migawanyiko ya kijiografia, matishio ya kinyuklia na utengenezaji wa silaha mpya za kisasa na uwekezaji wa fedha kwenye uharibifu na vifo badala ya kuleta matumaini na fursa mpya.
Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kitaifa, Balozi Thabit Kombo, Waziri wa Nchi (OR-Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo na Waziri wa Afya wa SMZ, Nassor Ahmed Mazrui na watendaji wengine wa Seikali.
Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ni “Hakuna kuachwa nyuma yeyote: Kushirikiana pamoja kuendeleza amani, maendeleo endelevu na heshima ya binadamu kwa vizazi vya sasa na vijavyo” (Leaving no one behind: Acting together for the advancement of peace, sustainable development and human dignity for present and future generations).