Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Masoko Mapya ya Madini  Yaingiza Bilioni  34.3 Kwa Mwezi Mmoja
May 27, 2019
Na Msemaji Mkuu

 

Na Frank Mvungi

Dhahabu ya Bilioni 34.3 imeuzwa katika kipindi cha mwezi mmoja kupitia katika masoko  21 yaliyoanzishwa kwa ajili ya kuuza madini katika mikoa mbalimbali hapa nchini. Akizungumza katika mahojiano maalum  na idara ya habari MAELEZO, Bungeni  Jijini Dodoma Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko amesema kuwa kuanzishwa kwa masoko hayo kumekuwa chachu ya kuongeza mchango wa sekta ya madini katika kukuza uchumi na pato la Taifa kwa ujumla. “ Katika kipindi cha mwezi mmoja tu yaani Machi 17 mpaka Aprili 17 mwaka huu,jumla ya kilo 409.3 za dhahabu pekee zenye thamani ya shiilingi bilioni 34.3 imeuzwa kupitia katika maduka yaliyoanzishwa katika mikoa mbalimbali” Alisisitiza Biteko. “katika kilo hizo,Mkoa wa Geita umeongoza kwa kufanya biashara ya  jumla ya kilo 289,Kahama kilo 44,Mara kilo 13,lakini cha kufurahisha zaidi ni  kwa Wilaya ya Chunya ambako jumla ya kilo 52 zimeuzwa katika soko hilo zikiwa nia siku chache toka kufunguliwa kwake ,”,aliongeza, mheshimiwa Biteko. Aidha mheshimiwa Biteko, katika mahojiano hayo maalum,ameeleza kuridhishwa na biashara inayofanyika katika maduka hayo ya madini kote nchini na kueleza kuwa licha ya mafanikio hayo yaliyofikiwa katika kipindi kifupi,serikali inashughulikia changamoto ndogondogo ikiwemo wafanyakazi,mashine za XRF na idadi ya watoa vibali. Akifafanua amesema kuwa  dhamira ya Serikali ni kuona sekta hiyo inatoa mchango stahiki  katika kujenga uchumi na kuchangia maendeleo hapa nchini ndio sababu mkazo umewekwa katika kusimamia sekta hii. Pia aliwataka wachimbaji wadogo na madalali wa madini kuhakikisha kuwa wanatumia masoko hayo kikamilifu  na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufutiwa leseni jambo alilosema serikali haipendi, Akizungumzia mikakati ya kusimamia sekta hiyo Mhe. Biteko amesema kuwa ni pamoja na kushirikisha wachimbaji wadogo katika kuhakikisha kuwa vitendo vya utoroshaji wa madini unakomeshwa ili kulinda mapato ya Serikali. Aliongeza kuwa hatua nyingine ni usimamizi wa karibu katika maeneo yote ya uzalishaji wa madini ya aina mbalimbali na kuchukua hatua za kutatua changamoto mbalimbali katika sekta hiyo. Katika mwaka wa fedha 2019/2020 Waziri Biteko amebainisha kuwa masoko mengine 7 yanatarajiwa kufunguliwa. Baadhi ya Mikoa ambayo imeshafungua masoko ya kuuza madini ni pamoja na Geita, Dodoma, Mwanza, Tabora, Shinyanga, Morogoro, Mbeya, ambapo tayari mikoa 21 imeshafungua maduka hayo hadi sasa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli alilolitoa kwa wakuu wa mikoa wote hapa nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi