Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mashirika yasiyo ya kiserikali yapewa siku 30 kuwasilisha taarifa za matumizi ya fedha na miradi kwa mwaka 2016 na 2017
Sep 29, 2018
Na Msemaji Mkuu

 

TARIFA KWA UMMA

MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI YAPEWA SIKU 30 KUWASILISHA TAARIFA ZA MATUMIZI YA FEDHA NA MIRADI KWA MWAKA 2016 NA 2017

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni miongoni mwa nchi nyingi duniani zinazozingatia misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku. Misingi ya Utawala bora pamoja na mambo mengine inasisitiza uzingatiaji wa masuala ya uwazi na uwajibikaji katika utendaji kazi wa kila siku jambo ambalo Serikali yetu imekuwa ikilihimiza na kulitekeleza ipasavyo. Tunapenda kufahamisha umma kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayatambua Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kuwa wabia muhimu katika kuleta maendeleo ya kijamii na Taifa.  Kutokana na umuhimu huo, Wizara ya Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekuwa ikisajili, kuratibu na kufuatilia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kuweka mazingira wezeshi kwa mashirika hayo kutoa mchango katika maendeleo ya jamii na Taifa letu. Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Mwaka 2001 inasisitiza misingi ya uwazi na uwajibikaji kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Aidha, Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Na. 24 ya mwaka 2002 ikisomeka pamoja na Marekebisho yake ya mwaka 2005 katika Kifungu cha 29 (a) na (b), Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yana wajibu wa kuwasilisha taarifa za kazi na fedha kila mwaka kwa Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kwa umma. Hata hivyo, takwa hili la kisheria limekuwa halizingatiwi ipasavyo. Vile vile, Kanuni za Maadili za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs Code of Conduct, GN. No. 363, 2008) ambazo zimeundwa kwa mujibu wa kifungu Namba 27 zinasisitiza uzingatiaji wa misingi ya uwazi na uwajibikaji katika utendaji kazi, usimamizi wa masuala ya fedha na utawala. Hali kadhalika, wanufaika wa miradi hiyo, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa wanamofanyia kazi na vyombo vya habari wanayo haki pia ya kupata taarifa za shughuli zao. Aidha, NGOs pia zinatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia Sera na vipaumbele vya nchi katika maeneo wanayofanyia kazi. Hata hivyo, baadhi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali hapa nchini yamekuwa hayazingatii wajibu wao wa kisheria kama nilivyoeleza hapo juu. Hali hii imekuwa ikizusha malalamiko na manunguniko kutoka kwa wananchi na baadhi ya wabia wetu wa maendeleo wanaotoa fedha zao kuchangia katika juhudi za nchi na wananchi kujiletea maendeleo. Kutokana na hali hiyo, Serikali inaagiza yafuatayo:
  1. Mashirika yote Yasiyo ya Kiserikali kuwasilisha kwa Msajili wa NGOs Taarifa za fedha (Audited financial statements) za miaka miwili iliyopita (2016 na 2017), wakati huo wanajiandaa kutoa taarifa ya mwaka 2018 mwishoni mwa mwaka huu.
  2. Mashirika yote kuwasilisha taarifa za vyanzo vya fedha, matumizi yake na miradi iliyotekelezwa na inayotarajia kutekelezwa kwa kipindi husika.
  • Kuwasilisha mikataba/ hati za makubaliano ya ufadhili wao kwa kipindi cha mwaka 2016 hadi sasa.
  1. Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yahakikishe kuwa miradi wanayoitekeleza inazingitia vipaumbele, mipango na mikakati ya Serikali katika ngazi ya Taifa, Mikoa na Wilaya ili kutoa mchango katika kufikia maendeleo endelevu kwa manufaa ya jamii na Taifa.
  2. Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yahakikishe kuwa kabla ya kutekeleza miradi yao ni sharti kuwasiliana na Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambaye yuko Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto sanjari; na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupata kibali ili kufanikisha jukumu la uratibu, ushirikishwaji na ufuatiliaji wa kazi za NGOs katika ngazi mbalimbali.
  3. Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Kimataifa (INGOs) yazingatie ushiriki wa wananchi na Mashirika ya ndani katika miradi wanayoitekeleza kwa mujibu wa Sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa shughuli za NGOs hapa nchini.
  • Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaliyosajiliwa chini ya Sheria nyingine, mfano Sheria ya Makampuni Na.12 ya mwaka 2002; Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini; Registration Insolvency and trusteeship Agency (RITA), Sheria ya Usajili wa Vyama vya Kijamii, Sura ya 337 ya Mwaka 2002  yanapaswa kuomba kupata cheti cha ukubalifu kwa mujibu wa kifungu 11 cha Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2005. Aidha, kufanya kazi pasipo kusajili chini ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni kosa kwa mujibu wa Sheria.
  • Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yatume taarifa zao za fedha na miradi za kila mwaka kupitia barua pepe ifuatayo dngo@communitydevelopment.go.tz, au kuleta taarifa zao moja kwa moja kwenye ofisi ya Msajili wa NGOs.
Maagizo niliyotaja yanatekelezwa ndani ya kipindi cha siku thelathini (30) kuanzia tarehe ya agizo hili na baada ya kipindi husika kukoma, Serikali itaanza kufuatilia na kuchukua hatua stahiki za kisheria ikiwa ni pamoja na kufuta usajili kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yatakayoshindwa kutekeleza agizo hili. IMETOLEWA NA: Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, DODOMA 28/9/2018    

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi