Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema mafanikio yaliyopatikana katika miaka 60 ya muungano ni kuanzisha madawati ya jinsia na watoto 420 nchi nzima ambayo yanasaidia kupambana dhidi ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto nchini.
Akieleza hayo leo jijini Dodoma, Waziri Masauni amefahamisha kuwa madawati hayo yamesaidia kuongezeka kwa uelewa wa wananchi juu ya maana, aina na madhara ya ukatili wa kijinsia pamoja na jinsi ya kuzuia matendo hayo ya kinyama.
"Uanzishwaji wa madawati ya jinsia na watoto umesaidia kuandaa askari wenye mafunzo maalum ya kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto kwa makundi yote katika jamii. Kupitia madawati haya, huduma bora ya namna ya kuwahudumia waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia imewezeshwa," ametaarifu Waziri Masauni.
Pamoja na hilo, Waziri Masauni amesema Polisi jamii imelisaidia Jeshi la Polisi kuwa na uwezo zaidi wa kubaini na kuzuia uhalifu na kuweka mazingira rafiki baina ya polisi na wananchi katika kupata taarifa za matukio mbalimbali kwenye jamii na kuongeza ufanisi katika majukumu yao.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unatimiza miaka 60 tangu ulipoasisiwa Aprili 26, 1964 na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.