Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Marufuku Waganga wa Jadi Kupokea Wagonjwa Wasio na Ripoti za Hospitali
Apr 17, 2020
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_52187" align="aligncenter" width="750"] Wajumbe wa Kamati ya Amani Mkoa wa Songwe walipokutana kujadili hatua zaidi za tahadhari ya ugonjwa huo ambapo moja ya hatua waliyokubaliana ni kutorusu waumini wengi katika nyumba za Ibada.[/caption]

Katika jitihada za kupambana na Ugonjwa wa Corona, Chifu wa Mkoa wa Songwe Mbeshena Nzunda amepiga marufuku kwa Waganga wa Jadi kupokea mgonjwa yeyote ambaye hana ripoti itakayo onyesha tatizo husika limeshindwa kutatuliwa hospitalini.

Chifu Nzunda amebainisha hayo katika kikao cha Kamati ya Amani ya Mkoa ilipokutana kujadiliana hatua zaidi za tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa na Mkoa wa Songwe ili kupambana na ugonjwa wa Virusi vya Corona.

Amesema ili mgonjwa apate matibabu kwa mganga wa jadi anapaswa kuonyesha ripoti kuwa baada ya kutibiwa hospitalini hakupona na  wataalam wa afya wathibitishe hilo pia waganga wa jadi wenye wateja wengi wanapaswa kuwahudumia kwa awamu ili kepusha msongamano.

Chifu Nzunda ameeleza kuwa waganga wa jadi wanatakiwa kuchukua tahadhari za ugonjwa huo kwa kunawa mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni pia kuweka maji hayo kwa ajili ya wateja watakaowahudumia.

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Songwe, Sheikh Hussein Issa akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo ambapo wamekubaliana kutoruhusu watoto katika nyumba za ibada ikiwa ni hatua mojawapo ya tahadhari zaidi juu ya ugojwa wa Corona.

Ameongeza kwa kuwataka watumiaji wa pombe za kienyeji kuhakikisha hawachangii vyombo vya kunywea pombe kama ilivyozoeleka bali kila mmoja awe na chombo chake, pia wauzaji  pombe hizo wachukue tahadhari kwa kuweka  maji ya kunawa na kupunguza misongamano.

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Songwe Sheikh Hussein Issa amesema kamati hiyo imekubaliana kuchukua baadhi ya hatua ikiwa ni kuongeza tahadhari zaidi ya ugonjwa huku uongozi wa Mkoa ukipongezwa kwa jitihada zilizochukuliwa kwani hadi sasa hakuna mgonjwa wa Corona.

Sheikh Issa amesema kuanzia sasa watoto wasiruhusiwe kushiriki katika nyumba zozote za ibada ili kuwaondoa katika hatari ya maambukizi ya Corona pia wazazi wahakikishe watoto wanabaki majumbani.

Ameongeza kuwa nyumba zote za ibada zisiruhusu waumini wengi kujaa bali waingie wachache na wakae mbalimbali bila kusongamana pia maji tiririka ya kunawa na sabuni au vitakasa mikono viwekwe ndani na nje ya nyumba hizo za Ibada.

Sheikh Issa amesema viongozi wote wa dini mbalimbali wanapaswa kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa huo kwa kufuata maelekezo ya Serikali pia wasiache kumuomba Mungu ili ugonjwa wa Corona usilete maafa katika Nchi ya Tanzania.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ameipongeza kamati hiyo kwa hatua hizo za tahadhari ya Corona huku akimuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa huo kuhakikisha anatoa elimu ya tahadhari ya Corona katika nyumba zote za Ibada.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi