Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Marufuku Kuruka Nyumba Uunganishaji Umeme wa REA
Apr 18, 2018
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_30523" align="aligncenter" width="1000"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye miwani) na Mbunge wa Urambo Magreth Sitta na viongozi wengine wakikata utepe wa uzinduzi wa uwashaji wa umeme wa REA katika Kijiji cha Jionee Mwenyewe kata ya Songambele jana.[/caption]

Na Tiganya Vincent - RS TABORA

SERIKALI imesema ni marufuku kwa Wakandarasi na Wataalamu kuruka nyumba wakati wa uunganishaji wa umeme kwa wananchi kupitia Mradi kabambe wa kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu unatekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

Kauli hiyo ilitolewa jana wilayani Urambo na Kaliua na Waziri wa  Nishati Dkt. Medard Kalemani wakati alipokuwa akikagua utekelezaji wa zoezi la usambazaji wa umeme wa REA katika maeneo hayo.

Alisema ni marufuku kuruka nyumba hata kama ni nyasi kama mwananchi anataka umeme na amelipa shilingi 27,000 za kuunganishiwa umeme.

Kalemani alisema kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha umeme unafika katika vijiji na vitongoji vyote na kwa wananchi wote bila kubagua.

[caption id="attachment_30528" align="aligncenter" width="1000"] Baadhi ya wanakijiji wa Jionee Mwenyewe Kata ya Songambele wakisikiliza Hotuba ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo katika picha ) mara baada ya kuzindua uwashaji wa umeme katika Kijiji chao jana. Picha na Tiganya Vincent - RS Tabora[/caption]

“Nawaagiza Wakandarasi na Wataalamu wote hakuna kuruka nyumba wala kubagua nyumba kwa sababu ya kuwa imeezekwa kwa nyasi, umeme ni nyumba kwa nyuma, kaya kwa kaya hata kama mtu hajakamilisha nyumba yake kama kuna mti karibu na nyumba yake wekeeni hata hapo ili iwe rahisi kuingiza umeme atakapokuwa amekamilisha nyumba yake” alisisitiza Waziri huyo.

Alisisitiza kuna mtindo wa Wakandarasi kuchagua nyumba wakati wanapotekekeza majukumu yao ya kuwaweka umeme, na kusema kuwa kwa hivi sasa hilo ni marufku umeme ni kwa wote wanaotaka.

Waziri huyo wa Nishati aliongeza kuwa ni marufuku kuwatoza wananchi wanaotaka kuunganishiwa umeme zaidi ya shilingi 27,000/- na kutoa wito kwa mwananchi kuwa atakayetozwa zaidi ya kiasi hicho atoe taarifa ili hatua kali dhidi ya wahusika ziweze kuchukuliwa.

Aidha alitoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa hiyo ya kuunganishiwa kwa gharama hizo kwani baada ya hapo itabidi walipie kulingana na taratibu za Shirilka la Ugavi wa umeme Tanzania (TANESCO)

Katika hatua  nyingine Waziri huyo wa Nishati amempongeza Diwani wa Kata ya Vumilia wilayani Urambo, Kassim Shushu kwa kutoa eneo lake kwa ajili ya kuwapatia TANESCO ili wajenge kituo cha kupozea umeme.

Alisema kitendo hicho cha Diwani wa Kata ya Vumilia kupitia ACT Wazalendo ni cha kizalendo na kimeonyesha kuwa maendeleo hayana chama na baada ya kukamilisha mradi TANESCO itabidi waone jinsi ya kumpa mkono wa shukrani.

Dkt . Kalemani alisema  baada ya Shirika lake la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) litajenga Kituo kidogo cha kupozea umeme (sub station) katika Kijiji hicho cha Uhuru ili  kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme kwa wananchi wa Wilaya ya Kaliua na Urambo na maeneo jirani.

Alisema Kituo kingine kitajengwa mpakani mwa Tabora na Kigoma kwa ajili ya kuuwezesha Mkoa wa Kigoma kuwa na umeme wa uhakika.

Waziri huyo wa Nishati alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza tatizo la kukatika kwa umeme katika maeneo hayo.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi