Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Maonesho ya Nane Nane Kitaifa Kufanyikia Simiyu
Jul 08, 2020
Na Msemaji Mkuu

Na Mathias Canal - Songwe

Serikali imetangaza kuanzia tarehe 01 hadi 08 Agosti, 2020 kutafanyika maadhimisho ya sikukuu ya wakulima nanenane ambapo kitaifa yatafanyika katika viwanja vya Nyakabindi, Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.

Akizunguzma na Waandishi wa Habari katika ziara ya kikazi mkoani Songwe, Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga amesema kuwa maonesho hayo yataambatana na uhamasishaji wa matumizi ya teknolojia bora za kilimo, ufugaji na uvuvi.

Pia, maonesho hayo yatashirikisha Wadau mbalimbali zikiwemo Wizara, Taasisi za Umma na Binafsi, Wabia wa maendeleo, wakulima na Vyama vya wakulima, wafugaji na wavuvi.

Waziri Hasunga amesema kuwa maonesho hayo ya Ishirini na Nane (28) tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993 yatafanyika kwenye Kanda nane (8) za Maonesho ambazo ni Kanda ya Mashariki (Morogoro), Kanda ya Kaskazini (Arusha), Kanda ya Magharibi (Tabora), Kanda ya Kusini (Lindi), Kanda ya Kati (Dodoma), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kanda ya Ziwa Mashariki (Simiyu) na Kanda ya Ziwa Magharibi (Mwanza).

Mhe. Hasunga amesema kuwa Kupitia maonesho hayo, viongozi mbalimbali wa Kitaifa watatembelea viwanja vya maonesho na kuhamasisha masuala mbalimbali ya kuendeleza sekta za kilimo, mifugo, uvuvi pamoja na Ushirika.

Amewataja baadhi ya viongozi wanaotarajiwa kushiriki katika maonesho hayo ngazi ya Taifa ni Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kadhalika amelitaja lengo la maonesho hayo katika kanda hizo kuwa ni pamoja na kutoa fursa kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wanaushirika kuona na kujifunza matumizi ya teknolojia bora za kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya kuongeza tija na uzalishaji kwa uhakika wa chakula, kukidhi mahitaji ya viwanda na masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kaulimbiu ya maonesho hayo kwa mwaka 2020 yamepambwa na kauli mbiu isemayo “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora 2020“.

Waziri Hasunga amebainisha kuwa mwaka 2020 ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, Kaulimbiu hiyo inatoa hamasa kwa wananchi kuchagua viongozi bora watakaokuwa chachu ya kuleta mapinduzi kwa ajili ya maendeleo ya sekta za kilimo ili kuinua ustawi wa maisha ya wakulima, wafugaji na wavuvi.

Aidha, Mhe Hasunga ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya umma na binafsi kukamilisha maandalizi ya kushiriki katika viwanja vyote vya maonesho vilivyopo kwenye Kanda Nane (8) kama nilivyoeleza hapo juu

Aidha, Kamati za Maandalizi ya Nanenane ngazi ya Kanda zinazoongozwa na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa zihakikishe zinakamilisha maandalizi yote muhimu na kuwashirikisha wadau wote.

Katika kuhakikisha Maonesho ya Kilimo yanakuwa na tija, Wizara ya Kilimo iliandaa na kusambaza katika mikoa yote Mwongozo wa Maonesho na Mashindano ya Kilimo, Mifugo Na Uvuvi. Mwongozo huo, pamoja na mambo mengine unaeleza Utaratibu wa Kusimamia na Kuratibu Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ikiwemo majukumu ya kila mdau; Matumizi Endelevu ya Viwanja Vya Maonesho;


Mapato na Matumizi kwa ajili ya Maonesho; na Ufuatiliaji na Tathmini. Hivyo, nisisitize Uongozi wa Mikoa katika Kanda zote uhakikishe kuwa Maonesho ya Nanenane yanafanyika kwa kuzingatia Mwongozo huo.

Kadhalika, amesema kuwa ni lazima mikoa ihakikishe viwanja vya Maonesho vinatumika muda wote kabla, wakati na baada ya maonesho kama mashamba darasa na vitovu vya kutoa elimu ya matumizi bora ya teknolojia bora za uzalishaji na masoko.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi