Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mamia ya Watanzania Wajitokeza Kupata Vyeti vya Kuzaliwa Sabasaba
Jul 08, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Lilian Lundo – MAELEZO

Mamia ya Watanzania wamejitokeza kujisajili kwa ajili ya kupata vyeti vya kuzaliwa katika banda la maonesho la taasisi ya Wakala wa Usajili na Udhamini (RITA) katika maonesho ya kimataifa ya 46 ya biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro ameshuhudia umati huo wa watu alipotembelea banda la RITA, leo Julai 6, 2022 kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi ndani ya viwanja vya Sabasaba.

“Leo nimetembelea banda la RITA, ambayo ni moja ya taasisi zilizopo katika Wizara ya Katiba na Sheria, nimekuta kuna umati mkubwa wa watu. Kwa mujibu wa taarifa nilizopewa, zaidi ya watu 1,000 wanakuja kujipatia huduma zao hapa kila siku,” alifafanua Dkt. Ndumbaro.

Aliendelea kusema kuwa, asilimia kubwa ya Watanzania waliojitokeza ni kwa ajili ya usajili wa vizazi na huduma nyingine zinazotolewa na RITA. Aidha amewataka Watanzania wanaohitaji vyeti vya kuzaliwa kufika katika viwanja vya Sabasaba, banda la RITA ili waweze kupata huduma hiyo.

Dkt. Ndumbaro amewapongeza Wafanyakazi wa RITA kwa kufanya kazi bila kupumzika masaa yote. Aidha, amewataka wafanyakazi hao kuendelea kuwahudumia Watanzania kama ambavyo Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan alivyowaagiza kuwahudumia Watanzania.

Kwa upande wake, Kabidhi Wasii Mkuu na Mtendaji Mkuu wa RITA, Angela Anatory amesema kuwa watu wengi wanajitokeza kufanya usajili katika maonesho ya Sabasaba kwa sababu wanapata huduma nyingi katika eneo moja.

“Kila ambapo tunapokuwa na matukio kama haya, Sabasaba na Nanenane tunatoa huduma, lakini pia huduma hizi zinatikana maofisini, kama vile makao makuu ya RITA, ofisi za wakuu wa wilaya, lakini pia kampeni kama hizi huwa tunazifanya mashuleni, na katika vituo vya afya vinavyotoa huduma ya mama na mtoto kwa ajili ya kuwasajili watoto chini ya miaka Mitano,” alifafanua Angela.

Aliendelea kusema kuwa, kwa sasa huduma ya kupata vyeti vya kuzaliwa inapatikana pia kwa njia ya mtandao, ambapo muombaji anatakiwa kujaza fomu ya maombi ya usajili inayopatikana katika tovuti ya RITA na kuituma bila kufika ofisi za RITA.

Aidha amesema kuwa, taasisi hiyo imesajili zaidi ya Watanzania 2800 kuanzia tarehe Juni 28, 2022 yalipoanza maonesho hayo ya Sabasaba mpaka Julai 5, 2022.

Wananchi wengi waliofika katika banda la RITA kwa ajili ya usajili wa vyeti vya kuzaliwa, wamefurahia huduma hiyo namna ambavyo imekuwa rahisi na ya haraka tofauti na walivyotegemea.

“Nimekuja kufanya usajili kwa ajili ya kupata cheti changu cha kuzaliwa, ili niweze kujiandikisha kupata kitambulisho cha Taifa. Huduma ni nzuri, kwani nimefika leo na nimefanikiwa kukamilisha taratibu zote, nasubiri kufuata cheti changu baada ya siku 10,” alifafanua Aisha Abdallah kutoka Chanika.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi