Ujumbe wa watu sita kutoka Makumbusho ya Taifa ya Oman umetembelea Makumbusho ya Taifa Dar es Salam kwa ajili ya kujifunza na kujionea historia ya Tanzania.
Ujumbe huo unaongozwa na Mtendaji Mkuu wa Makumbusho ya Taifa ya Oman, Mheshimiwa Jamal al-Moosawi. Pamoja na mambo mengine, ujumbe huo unatarajia pia kutembelea Kijiji cha Makumbusho Kijitonyama, Jumba la Atiman na Jengo la Boma la zamani yaliyoko katika Mtaa wa Sokoine ambapo majengo hayo yaliyojengwa na kukaliwa na Sultan wa Zanzibar miaka ya 1860.
Ujumbe huo kutoka Makumbusho ya Taifa ya Oman unatarajia kutembelea visiwa vya Zanzibar ambapo watakutana na kuzungumza na uongozi wa watendaji wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale iliyo chini ya Wizara ya Utalii na Urithi Zanzibar.
Ukiwa Zanzibar Ujumbe huo utatembelea Mji Mkongwe, Makumbusho ya amani na historia ya Mnazi Mmoja, Jumba la Kibweni na Magofu ya Mtoni. Ujumbe huo pia utatembelea Pango la Kuumbi la Jambiani, Makumbusho ya Unguja Kuu na Mji Mkongwe kwa ajili ya kujifunza na kujionea historia iliyosheheni ya Zanzibar.
Ujumbe huo kutoka nchini Oman uliwasili nchini tarehe 05 Oktoba, 2023 ambapo pamoja na mambo mengine, una shiriki Mkutano wa Kwanza wa Pamoja wa Wataalamu kati ya Tanzania na Oman unaofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo unalenga kuendeleza uhusiano kati ya Tanzania na Oman kupitia Makumbusho ya Taifa ya Tanzania na Makumbusho ya Taifa ya Oman.
Mkutano huo wa Kwanza wa Pamoja wa Wataalamu kati ya Makumbusho ya Taifa ya Tanzania na Makumbusho ya Taifa ya Oman ni moja ya mbinu na nyenzo za kuimarisha Uhusiano kati ya Tanzania na Oman.
Kufanyika kwa Mkutano huo ni utekelezaji wa makubaliano yaliyosainiwa kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Makumbusho ya Taifa ya Oman mwezi Juni ,2022.
Ujumbe huo unatarajiwa kuondoka nchini tarehe 12 Oktoba 2023 kupitia Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar.