Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makandarasi Wazawa Wafundwa Kibiashara
Aug 02, 2023
Makandarasi Wazawa Wafundwa Kibiashara
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Mhandisi Rhoben Nkori, akizungumza na Makandarasi (hawapo pichani) waliokuwa kwenye mafunzo ya siku Tatu kuhusu masuala ya kibiashara kwa Makandarasi hao, Jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu

Makandarasi wazawa wametakiwa kuzisimamia kampuni zao kwa ufasaha kwa kufuata sheria za ulipaji wa kodi kwa wakati na kufanya kazi kwa weledi kwa kutumia wataalamu stahiki katika sekta mbalimbali ili kukwepa changamoto katika maeneo yao ya kazi.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo yenye lengo la kuwajengea uwezo Makandarasi wazawa kibiashara, jijini Dodoma, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Mhandisi Rhobin Nkori, alisema kuwa lengo mojawapo la kufanya mafunzo hayo ni pamoja na kutoa elimu kwa makandarasi kuhusiana na mvutano baina yao na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Nimefurahi kuona kwamba moja ya mada itakayofundishwa ni kuhusu masuala ya kodi kwa makandarasi, hii itatusaidia kupunguza matatizo makubwa sana kati ya wakandarasi na TRA”, alisema Msajili.

Baadhi ya Wakandarasi wakimsikiliza Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Mhandisi Rhoben Nkori (hayupo pichani), wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku Tatu kuhusu masuala ya kibiashara kwa Makandarasi hao, Jijini Dodoma .

Aidha, Mhandisi Nkori, alisema makampuni mengine hutumika kufanya kazi kwa majina ya wamiliki wengine yanayopelekea mvutano pindi kazi inapoenda kukaguliwa na TRA kupitia Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), hivyo amewataka wamiliki wa makampuni kusimamia vyema makampuni yao ili kuepuka changamoto hizo.

Mhandisi Nkori amesisitiza kuwa ili kuendelea kujenga taswira nzuri kwa makandarasi nchini, Bodi itaendelea kuwachukulia hatua kisheria makandarasi wote wanaokiuka maadili yao ya kazi.   

Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Mhandisi Rhoben Nkori (wanne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na makandarasi mara baada ya kufungua mafunzo ya kibiashara kwa makandarasi hao yaliyofanyika jijini Dodoma.

Naye, Mkurugenzi wa kampuni ya SONCO ENGINEERING COMPANY LIMITED, Mhandisi Baraka Materu, ameiomba serikali kuweka mikakati maalumu ya kuwashirikisha wakandarasi wazawa wakati wa utekelezaji wa miradi mikubwa ili kuwajengea uwezo makandarasi hao kutokana na teknolojia mpya ambayo watajifunza kupitia miradi hiyo.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanayotolewa na Bodi hiyo yameshirikisha makandarasi kutoka sehemu mbalimbali nchini lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu na kuwajengea uwezo makandarasi hao katika mujukumu yao ya kazi. 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi