Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais kuhamia Dodoma Huu, Rais Kuhamia 2018 - Magufuli
Sep 23, 2017
Na Msemaji Mkuu

Rais Atangaza Ajira Mpya 50,000 Zikiwemo 3000 za Jeshini

Na:  Prisca  Libaga, MAELEZO -  Arusha.

Rais John Pombe Magufuli amesisitiza azma ya Serikali kuhamia Dodoma ambapo amesema kuwa mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka huu, Makamu wa Rais atakuwa amehamia Dodoma na kufikia mwakani yeye mwenye Rais atakuwa amehamia pia.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo jijini Arusha baada ya kuwatuniku nishani ya Cheo cha Luteni Usu Maafisa wapya 422 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania, ambapo 314 kati yao wamehitimu katika Chuo Cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA) na 84 kwenye shule ya Ubaharia wa Kijeshi, Kigamboni huku 14 wakitokea shule ya Urubani wa Kijeshi Ngerengere, mkoani Morogoro na 10 wakiwa wamehitimu vyuo vya nje.

“Waziri Mkuu Kassim Majaliwa tayari amekwisha kuhamia Dodoma. Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu yeye anaondoka Dar-es-salaam mwaka huu na mimi mwenyewe pamoja na ikulu yote tutahamia Dodoma mwaka 2018,” alisema Rais Magufuli.

Alieleza kuwa kama kuna wizara au mfanyakazi wa Serikali ambaye ataendelea kung’ang’ania jijini Dar-es-salaambaada ya viongozi wote wakuu kuhamia Dodoma basi ajihesabu kuwa hana kazi tena.

“Hatuwezi kuendelea kuvutana na hili suala la kuhamia Dodoma wakati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alishafanya uamuzi huu tangu mwaka 1973,” alisema Rais Magufuli na kusisitiza kuwa imefika wakati wa Serikali na vyombo vyake vyote muhimu vianze safari ya kwenda Dodoma.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amesema kuwa Serikali inatarajia kutoa ajiza 50,000 ili kuziba mapengo yalioachwa wazi wakati wa zoezi la kuwaondoa watumishi hewa ikiwa ni pamoja na wale waliokosa sifa.

Rais Magufuli pia ameiagiza wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kuhakikisha kuwa linatoa kipaumbele kwa wahitimu wote wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika ajira 3000 zinazotarajiwa kutolewa na jeshi hilo.

 Wakati huo huo, Rais Magufuli amesema tayari serikali imefanikiwa kuziba mianya yote ya upotevu wa fedha kiasi kwamba mapato ya taifa kwa mwaka yameongezeka kutoka Bilioni 800 hadi Trilioni 1.3 na yanaendelea kupanda.

Halafu kutokana na fedha hizo, serikali inatumia asilimia 40 kwenye miradi ya maendeleo kama afya, elimu na maji ambayo hugharimu zaidi ya Billioni 520 kwa mwaka.

“Na kwa hapa Arusha tayari mradi mkubwa wa maji wa billioni 16 umezinduliwa Longido juzi, huku barabara ya njia nne kuunganisha jiji na eneo la Tengeru ikiwa nayo imekamilika na tunatarajia kujenga barabara nyingine kubwa ya mzunguko kutoka Ngaramtoni hadi Usa-River.”

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi