Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais, Dkt. Mpango Awasili Jijini Arusha Tayari kwa Uzinduzi wa Kongamano la Kiswahili Duniani
Mar 13, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Eleuteri Mangi-WUSM, Arusha

Makamu wa Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango leo Machi 13, 2022 amewasili jijini Arusha tayari kwa ufunguzi wa Kongamano la Pili la Idhaa za Kiswahili duniani litakalofanyika Machi 14, 2022 katika Ukumbi wa Kimataifa (AICC) jijini Arusha.

Kongamano hilo linawakutanisha pamoja Waandishi wa Habari na Watangazaji wa Idhaa zinazotumia lugha ya Kiswahili duniani kubadilishana uzoefu katika shughuli zao za kihabari ili kuleta tija zaidi katika kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha jamii.

Hadi sasa washiriki kutoka vyombo vya habari mbalimbali vya ndani na nje ya nchi wamethibitisha kushiriki kongamano hilo ambapo zipo redio za hapa nchini ni 45, redio za nje ni 15, televisheni za kawaida na za mtandaoni ni 13, televisheni za nje ya nchi mbili, wahadhiri wa vyuo vikuu vya ndani 20, wachapishaji watano, watu mashuhiri kutoka ndani na nje ya nchi 16 pamoja na wanafunzi 200 kutoka vyuo vikuu vya jijini Arusha.

Washiriki wa Kongamano hilo wanatoka katika nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Malawi, Marekani, Rwanda, Ufaransa, Uganda, Ujerumani na wenyeji Tanzania.

Wazo la kuandaa Kongamano la Idhaa za Kiswahili Duniani lilianzishwa Novemba 29, 2006 na Kongamano la kwanza lilifanyika Novemba 12-15, 2007 ambapo lengo lake likiwa ni kuimarisha uhusiano na vyombo vya habari ambavyo vinatekeleza jukumu la kukieneza Kiswahili duniani kwa kukitumia katika kutangaza katika vituo vyao vya habari.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi