Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Dkt. Mpango Ameweka Jiwe la Msingi Kituo cha Afya Nsemulwa
Jul 21, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ameweka jiwe la msingi kituo cha afya Nsemulwa kilichopo Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi. Kituo hicho kilianza kujengwa mwaka 2021 kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Shilingi milioni 400 na kikitarajia kuhudumia wakazi zaidi ya 14,000 wanaoishi eneo hilo.

Mradi wa Ujenzi wa Kituo hicho cha Afya ulianzishwa na wananchi na umelenga kusogeza huduma za afya kwa wananchi na kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali teule ya Rufaa mkoani katavi.

Akizungumza na viongozi pamoja na wananchi wa Mpanda mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika kituo hicho cha afya, Makamu wa Rais amewapongeza wananchi wa Katavi kwa kudumisha amani pamoja na kufanya kazi kwa bidii katika nyanja mbalimbali ikiwemo kilimo iliopelekea kuzalisha chakula cha kutosha na ziada.

Amesema Serikali itaendelea kusogeza huduma muhimu kwa wananchi kama vile maji, elimu na afya katika jitihada za kuboresha maisha ya Watanzania. Ameongeza kwamba kwa sasa asilimia 90 ya dawa muhimu zinapatikana katika vituo vyote vya afya nchini na kuwapongeza wote walioshiriki katika ujenzi wa kituo hicho cha afya kwa kuiunga mkono Serikali katika utoaji wa huduma za afya.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekemea vitendo vya kuwakatisha wanafunzi wa kike masomo kwa kuolewa pamoja na kupata ujauzito. Amesema Mkoa wa Katavi unaongoza kwa asilimia 40 kuwa na mimba za utotoni na kuwataka watendaji wote wa Serikali, wazazi, viongozi wa dini na taasisi zote za kijamii kuungana kudhibiti vitendo hivyo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo Dugange amesema katika Manispaa ya Mpanda, Serikali imeendelea na ujenzi wa miradi yenye tija kwa wananchi kama vile ya afya, elimu na barabara. Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kutoa magari mawili ya wagonjwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kutokana na changamoto iliyopo ya upungufu wa magari hayo. Pia amesema pamoja na magari hayo, Serikali itapeleka mashine za X-ray nne katika mkoa huo ikijumuisha kituo cha afya cha Irembwe kilichopo Manispaa ya Mpanda itakayosaidia kupata huduma za kisasa za upimaji.

Awali Makamu wa Rais amezungumza na wananchi wa Kata ya Katumba Kijiji cha Msaginya Jimbo Msimbo ambao walisimama barabarani kumsalimia. Amewapongeza wananchi hao kwa kuendelea kufanya kazi za uzalishaji ikiwemo chakula na kuwaahidi kuwa serikali haitaacha kupeleka fedha katika vijiji hivyo ili kuimarisha maendeleo ya wananchi katika sekta mbalimbali kama maji, elimu, afya na barabara.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi