Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amewaasa watanzania waishio nchini Sweden pamoja na maeneo mengine duniani (Diaspora) kuwa na mshikamano pamoja na maelewano ili waweze kutatua changamoto zao zinazowakabili pamoja na kuchangia ujenzi wa taifa lao la Tanzania.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipofanya mazungumzo na viongozi na wawakilishi wa vyama mbambalimbali vya watanzania waishio nchini Sweden.
Amesema Serikali inathamini mchango mkubwa unaotolewa na diaspora katika kufanikisha adhma ya diplomasia ya uchumi hivyo wanapaswa kuondoa tofauti zao na kuendelea kuitangaza vema Tanzania nchini Sweden.
Pia, amewataka kuheshimu katiba za vyama vyao wanavyoviongoza nchini Sweden pamoja na kukutana na kujadili kwa uwazi kwa kuzingatia katiba waliojiwekea katika kuendesha mambo yao.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba Diaspora ni sehemu muhimu ya Tanzania, kwani serikali inathamini sana utaalamu, biashara na utangamano unaoleta manufaa kwa familia zao pamoja na taifa kwa ujumla.
Aidha, Makamu wa Rais amewahakikishia kuwa serikali inaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo za uwekezaji, utalii pamoja na biashara.
Amesema suala la Hadhi Maalum kwa wanadiaspora, Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kulifanyia kazi kwa kuzingatia maoni yaliotolewa na kuwaahidi suala hilo kushughulikiwa kikamilifu na kwa wakati.
Makamu wa Rais ameupongeza Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa watanzania waishio nchini Sweden na maeneo mengine ya uwakilishi.
Kwa upande wao, wawakilishi wa vyama mbalimbali vya wanadiaspora nchini Sweden, wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuteua watumishi waadilifu na wachapa kazi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden. Aidha wameiomba serikali kushughulikia kero mbalimbali zinazowakabili zikiwemo mazingira bora ya kufanya biashara, changamoto katika sekta ya utalii, pamoja na changamoto za huduma za kifedha wanazopata katika mabenki mbalimbali nchini Tanzania.
Aidha, wanadiaspora hao wamemueleza Makamu wa Rais jitihada mbalimbali wanazozifanya katika kuchangia ujenzi wa taifa kama vile uwekezaji katika sekta ya ufugaji, biashara, elimu pamoja na kilimo.