Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Azindua Huduma za Mawasiliano Kasumo Buhigwe
Dec 14, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango amewasihi watanzania kutumia vema mawasiliano katika kujiletea maendeleo ikiwa pamoja na kupata maarifa mapya ya kilimo na ufugaji pamoja na biashara.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizindua huduma ya mawasiliano katika kata ya Kajana Kijiji cha Kasumo Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, huduma iliyofikishwa na Shirika la Mawasiliano Nchini (TTCL) kwa kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF).

Amesema Serikali inaendelea kuboresha huduma za mawasiliano hasa maeneo ya mipakani ili kuharakisha maendeleo ya wananchi pamoja na kuongeza ulinzi na usalama katika maeneo hayo. Makamu wa Rais amesema uwepo wa huduma za intaneti hasa katika maeneo ya vijijini ni kichocheo kikubwa cha kuboresha huduma za kijamii pamoja na kufungua fursa za kiuchumi na kijamii katika taifa.

Amewasihi wananchi wa Vijiji vilivyonufaika na mawasiliano hayo kutumia katika kujitengenezea ajira ikiwemo kuanzisha biashara bunifu zinazotokana na uwepo wa mawasiliano.

Aidha, Makamu wa Rais amewataka wananchi wa Kasumo kutumia mawasiliano hayo kutoa taarifa muhimu zikiwemo za wahamiaji haramu, uhalifu pamoja na ajali za kimiundombinu kama ya umeme il

i kusaidia Serikali kuchukua hatua za haraka katika kukabiliana na changamoto hizo.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewataka wananchi wa maeneo hayo kulinda miundombinu ya mawasiliano iliyowekwa kwani kuhujumu miundombinu hiyo ni kujirudihsha nyuma kimaendeleo. Amesema Serikali inatumia gharama kubwa katika kuwafikishia wananchi mawasiliano hasa maeneo ya vijijini hivyo jukumu la ulinzi wa miundombinu hiyo ni la kila mwananchi.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na wote wanaotumia vibaya mawasiliano ikiwemo kufungia jumla ya laini za simu 64928 pamoja na kufungia namba za utambulisho 50703 ambazo zilizuiliwa kusajili kutokana na kutumika kusajili namba zilizoshiriki katika uhalifu.

Waziri Dkt. Kijaji amesema wizara itaendelea kulisimamia shirika kwa ukaribu ili liweze kujiendesha kwa faida ikiwemo kuongeza wateja wa ndani na nje ya nchi , kuongeza uwajibikaji katika kutoa huduma pamoja kuongeza mapato ya shirika na serikali kwa ujumla.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Nchini, Waziri Kindamba amesema TTCL imetatua changamoto kubwa iliowakabili wananchi wa Kasumo kwa muda mrefu ya kushindwa kutumia huduma za kifedha pamoja na Intaneti katika simu zao za mkononi.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF), Bi. Justina Mashiba amesema miradi ya mawasiliano inaendelea katika kata 1068 nchi nzima ili kuhakikisha maeneo ya vijijini na yale ya pembezoni mwa nchi yanapata mawasiliano.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi