Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Awataka Watumishi wa Ofisi Hiyo Kushirikiana na Wizara Zingine ili Kutekeleza Majukumu Yao kwa Ufanisi Zaidi
Mar 23, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 23 Machi 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ya Wizara hiyo Mtumba Jijini Dodoma.

Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais alipokea changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi hao pamoja na mapendekezo na maoni ya watumishi ya namna bora ya kutekeleza majukumu ya wizara hiyo yenye dhamana ya Mazingira na Muungano hapa nchini.

Akizungumza na watumishi hao, Makamu wa Rais amewataka kufanya kazi kwa bidii, nidhamu pamoja na kufuata kanuni na maadili ya Utumishi wa umma wakati wote wanapotekeleza majukumu yao. Aidha, amewataka kuwa na ushirikiano na Ofisi pamoja na Wizara zingine ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Amesema wajibu wa Wizara hiyo ni kuhakikisha inalinda na kudumisha  Muungano hivyo amewataka watumishi hao kushiriki vikao vya kamati ya pamoja vyote kama ilivyopangwa na kutatua changamoto zinazojitokeza pamoja na kuimarisha yale mazuri yote yanayohusu Muungano. Ameiagiza Wizara hiyo kuhakikisha inaongeza kasi ya utoaji elimu ya muungano kuanzia shule za msingi mpaka vyuo vikuu, kwa watumishi wa serikali pamoja na jamii kwa ujumla. Amesema jamii inapaswa kutambua sifa nzuri za muungano na kuitaka wizara kutumia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii pamoja na Sanaa.

Halikadhalika, amewataka watumishi wa Idara ya Mazingira kuhakikisha wanasimamia kikamilifu suala la mazingira ikiwemo upandaji miti pamoja na usafi wa mazingira. Amesema matatizo kama yaliyojitokeza mto Mara hivi karibuni na kusababisha vifo vya viumbe hai katika mto huo yanapaswa kutambulika mapema kufuatia ufuatiliaji wa karibu wa mazingira. Amewataka watumishi wa wizara hiyo kuwa wa mfano katika suala la upandaji miti na kuwataka kuchukua hatua binafsi za utunzaji mazingira katika maeneo wanayoishi.

Pia, Makamu wa Rais amewataka kuendelea kufuatilia maazimio ya kimataifa pamoja  na kuongeza ushirikiano na wadau wa mazingira, sekta binafsi, taasisi za kimataifa , dini pamoja na taasisi za fedha ili kupata teknolojia rahisi pamoja na upatikanaji wa fedha utakaowezesha kutekeleza program mbalimbali za mazingira.

Awali akimkaribisha Makamu wa Rais kuzungumza na watumishi hao, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jafo amesema Wizara itaendelea kuwa kioo katika suala la muungano na ajenda ya utunzaji mazingira pamoja ambapo tayari mafanikio yameanza kuonekana ikiwemo wananchi mbalimbali kuanza uuzaji na upandaji wa miti katika maeneo yao.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi