Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Atoa Pole Msibani kwa Malecela
Feb 20, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akiongozana na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango, leo tarehe 20 Februari 2022 wamefika nyumbani kwa Waziri Mkuu Mstaafu, Samwel Malecela Mtaa wa Kilimani Jijini Dodoma kutoa pole kufuatia kifo cha mtoto wake, Dkt. MweleNtuli Malecela kilichotokea tarehe 10 Februari 2022 Geneva nchini Uswisi.

Akitoa neno la faraja kwa familia na waombolezaji mbalimbali waliojitokeza nyumbani hapo, Makamu wa Rais amewasihi kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu pamoja na kumuombea marehemu apate pumziko la Amani. 

Makamu wa Rais amemtaja Dkt. Mwele kama shujaa aliejitoa kupigania Afya za wananchi wengine kupitia tafiti mbalimbali alizokuwa akizifanya zenye lengo la kusaidia jamii kupambana na magonjwa mbalimbali. 

Amesema Dkt. Mwele alifanya kazi iliyo njema na kuonekana katika jamii ndani na nje ya nchi.

Aidha, Makamu wa Rais amesema, katika kipindi cha uhai wake , Dkt. Mwele Malecela aliinua jina la Tanzania kwa kuaminiwa kufanya kazi katika taasisi kubwa ya afya duniani. 

Amesema uwezo wa Dkt. Mwele katika kazi pia uliinua wanawake hapa nchini hivyo hapana budi kumshukuru Mungu kwa zawadi hiyo pamoja kumuombea ampokee ili apumzike kwa Amani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi