Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Atembelea Kiwanda cha Scania Nchini Sweden
Jun 01, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango leo tarehe 1 Juni, 2022 ametembelea Makao Makuu ya kampuni ya utengenezaji wa magari ya Scania iliopo Stockholm nchini Sweden. 

Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais ameshuhudia teknolojia ya utengenezaji wa magari yanayotumia nishati ya gesi ikiwemo gesi inayotokana na taka ngumu inayotumiwa na kampuni ya utengenezaji magari yaScania kwa lengo la kupunguza ongezeko la gesi joto duniani.

Makamu wa Rais ameshiriki mazungumzo na Mkurugenzi wa Teknolojia endelevu ya utengenezaji magari wa Kampuni ya Scania, Jonas Strömberg pamoja na kuu wa Teknolojia endelevu ya usafirishaji wa kampuni ya Scania, Fredrik Wijkander, mazungumzo yaliyolenga kuongeza ushirikiano baina ya Tanzania na Kampuni hiyo.

Makamu wa Rais amesema Tanzania ipo tayari kwa ajili ya ushirikiano na kampuni hiyo hasa katika vyuo vya ufundi vitakavyowezesha uhamilishaji wa teknolojia. 

Aidha, ameikaribisha kampuni hiyo kushirikiana na Wafanyabiashara pamoja na Wawekezaji wa sekta ya usafiri waliopo Tanzania ili kueneza teknolojia ya matumizi ya nishati mbadala katika usafirishaji na kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wake Mkuu wa Teknolojia endelevu ya usafirishaji wa Kampuni ya Scania, Fredrik Wijkander amemshukuru Makamu wa Rais kwa kuitembelea kampuni hiyo na kuipongeza nchi ya Tanzania kwa kuendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na uharibifu wa mazingira. 

Amesema kampuni ya Scania inavutia na mabadiliko mbalimbali yanayofanyika nchini Tanzania ikiwemo uboreshaji wa sekta ya uwekezaji ambayo inawapa hamasa ya kushirikiana na Tanzania katika sekta ya usafirishaji hususani usafiri wa mizigo na abiria.

Makamu wa Rais yupo nchini Sweden kuhudhuria mkutano wa umoja wa Mataifa wa Stockholm +50 wenye dhumuni la kuchochea utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (Ajenda 2030) hususani katika upande wa mazingira na kujadili namna ya kurejesha uchumi endelevu katika kukabiliana na  janga la Uviko 19.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi