Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Serikali barani Afrika kuanzisha sera na sheria zitakazotoa uhuru kwa wakaguzi wa ndani ili waweze kutoa ushauri wa kweli na uhalisia.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa 10 wa Shirikisho la Taasisi za Wakaguzi wa Ndani Afrika (AFIIA) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC). Amesema serikali za Afrika zinapaswa kuwa na kifungu katika Sheria ya Ukaguzi wa Umma ambacho kitalinda Wakaguzi wa Ndani dhidi ya ushawishi au kuingiliwa katika majukumu yao isivyostahili.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba mfumo wa kisheria unaweza pia kuanzisha uhusiano katika utoaji taarifa za kiutendaji na kiutawala kwa wakaguzi wa ndani kwa kuzingatia Mfumo wa Kimataifa wa Mazoezi ya Kitaalamu (IPPF), kama suluhu ya uwezekano wa vitisho na vikwazo kutoka kwa baadhi ya Wakurugenzi Wakuu katika taasisi zao.
Aidha, Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa Serikali, Wakuu wa Mashirika ya Umma na Binafsi kutenga bajeti sahihi za mafunzo kwa ajili ya vijana wataalamu wa ukaguzi wa ndani ili kuwajengea uwezo zaidi katika utaalamu wao kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ukaguzi wa ndani na kutafuta njia sahihi za kuzitatua.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema kutokana na maendeleo ya kasi ya teknolojia hususani matumizi ya akili mnemba (AI), Wakaguzi wa Ndani wanahitaji kujipatia ujuzi wa hali ya juu zaidi wa kiteknolojia ili kuwawezesha kugundua, kuangalia na kudhibiti ukiukwaji wa taratibu. Amesema Wakaguzi wa Ndani wanapaswa kuendana na maendeleo ya haraka ya kiteknolojia, kurejea mifumo ya usimamizi wa taarifa, miundo ya uendeshaji na mikakati ya biashara ili kukabiliana na ongezeko la ukosefu wa usalama wa mtandao.
Pia Makamu wa Rais amewasihi Wakaguzi wa Ndani wote kuona wajibu wa kutekeleza majukumu yao kwa kutumia kanuni na viwango vya kimataifa. Amezihimiza Serikali za Afrika na Wadau kutoa msukumo wa kuidhinishwa kwa Wakaguzi wa Ndani kama ilivyo utaratibu wa kawaida katika taaluma zingine.
Makamu wa Rais amewataka washiriki wa mkutano huo kujadili changamoto zinazokabili mazingira kwa sasa duniani na hivyo kusaidia serikali na mashirika katika kupata ustahimilivu na kudhibiti athari zozote za kimazingira zinazojitokeza.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya amesema hali ya utawala, uthibiti and ukaguzi imeendelea kuimarika duniani ambapo uongozi wa kimataifa wa wakaguzi wa ndani unaongoza taasisi zake katika kuweka misingi na kulinda weledi.
Ameongeza kwamba nchini Tanzania katika sekta ya umma, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa pande zote mbili za Muungano ikiwa na wakaguzi zaidi ya 1,600 wanasimamia kuhakikisha wakaguzi wa ndani wanafuata misingi iliyowekwa ili serikali iweze kufikia malengo yake.