Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema katika kushughulikia changamoto za Kimataifa za uhaba wa chakula, Mabadiliko ya tabianchi pamoja na ukosefu wa ajira kwa vijana inahitajika juhudi za pamoja za wadau wote na uwepo wa amani endelevu Barani Afrika.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa 53 wa Mwaka wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika unaofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Gran Melia Jijini Arusha. Amesema Mabunge barani Afrika yana nafasi ya kipekee katika kufikia malengo hayo kwa kutunga sheria madhubuti na kufanya uangalizi.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa mkutano huo kutumika katika kubadilishana mbinu bora na uzoefu wa mataifa kukabiliana na changamoto mbalimbali kwa ufanisi zaidi sambamba na azimio la kumaliza migogoro na vita barani Afrika.
Kuhusu ajira kwa vijana, Makamu wa Rais amesema Mabunge yana wajibu wa kueleza changamoto za vijana, kuweka mbele hatua za kuchukuliwa na kushauri serikali katika kubuni programu za ajira kwa vijana na kuhakikisha kwamba zinafadhiliwa ipasavyo kupitia bajeti ya taifa na ushirikiano wa wadau mbalimbali. Ameongeza kwamba Mabunge yanapotunga sheria na kufanya usimamizi yanahitaji kufanya kazi na serikali ili kukuza sera na programu zinazounga mkono ajira na ufadhili wa kibunifu kwa programu za ujasiriamali kwa vijana.
Kuhusu Mabadiliko ya tabianchi, Makamu wa Rais amesema Wabunge wana wajibu wa kuhakikisha hatua madhubuti zinachukuliwa na serikali pamoja na wadau wengine ili kukabiliana na janga hilo kupitia utekelezaji wa hatua madhubuti ikiwemo za matumizi ya teknolojia za kijani. Pia amesema licha ya kutenga bajeti ya uhifadhi mazingira kitaifa ni muhimu mabunge kuharakisha uidhinishaji na utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ikiwemo Mkataba wa Paris pamoja na Marekebisho ya Doha kwa Itifaki ya Kyoto.
Aidha, Makamu wa Rais amesema Mabunge pia yanapaswa kusimamia utekelezaji wa mipango iliyoamuliwa kitaifa ili kupunguza uzalishaji wa gesi joto pamoja na kuimarisha uwazi na uwajibikaji wa hatua na utoaji wa taarifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi. Halikadhalika kuwa mstari wa mbele katika ajenda ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuandaa mijadala yenye ubora ili kukuza uelewa na hatua za kuchukua haraka kuzuia uharibifu wa mazingira kitaifa na kimataifa.
Vilevile akizungumzia uhaba wa chakula, Makamu wa Rais amesema licha ya uwezo mkubwa wa kilimo barani Afrika, bado wananchi wanakabiliwa na ukosefu wa chakula. Ametoa rai kwa Mabunge barani Afrika kuweka mkazo katika kuimarishwa kwa uwekezaji wa umma katika sekta ya kilimo na sekta shiriki kwa kutenga bajeti kwa ajili ya kuongeza usambazaji na upatikanaji wa pembejeo za kilimo na huduma za miundombinu.
Pia Makamu wa Rais amesema Mabunge yana jukumu la kutunga sheria zitakazosaidia usalama wa chakula na kuwezesha uwekezaji katika sekta ya kilimo na sekta shirikishi. Amesisitiza umuhimu wa miundombinu ya umwagiliaji, upatikanaji wa mikopo ya kilimo, mbegu bora, huduma za ugani, maghala ya uhifadhi mazao, huduma za miundombinu vijijini pamoja na upatikanaji wa masoko.