Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Afungua Kongamano la Kiswahili
Mar 14, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 14 Machi 2022 amefungua Kongamano la Pili la Idhaa za Kiswahili Duniani, ufunguzi uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Arusha (AICC).

Makamu wa Rais amewaasa wataalamu, mabingwa na wapenzi wa Lugha ya Kiswahili kuendelea kuandika vitabu vya taaluma mbalimbali kwa lugha hiyo ili kuepusha ongezeko la upotoshaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili miongoni mwa jamii husasani  wanahabari  wanaotumia maneno yasiyo rasmi au kuchanganya kiswahili na maneno ya lugha nyingine.

Amesema ubunifu unahitajika katika ufundishaji na uwasilishaji wa lugha ya Kiswahili kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ili kuendana na kasi ya maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Aidha, amesema katika tasnia ya habari, ni muhimu kuwa na vifaa bora vitakavyowezesha maarifa ya lugha hii yafike popote yanapohitajika kwa haraka na ufasaha.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ipo tayari kushirikiana na Taasisi na wadau mbalimbali katika kusimamia kwa karibu Mkakati wa Taifa wa kubidhaisha Kiswahili ambao utazinduliwa rasmi siku ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani na kuhakikisha kuwa unatekelezwa kikamilifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Amesema Serikali itaendelea kuhamasisha ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni kupitia Balozi na kujenga ushawishi kwa nchi nyingine kuingiza Kiswahili katika mitaala ili kuendelea kusambaza lugha hiyo.

Awali akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa amesema wizara itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wataalamu wa lugha ya kiswahili ili waweze kutumia fursa mbalimbali za lugha hiyo kama vile ukalimani, tafsiri, ufundishaji, uhariri na uandishi wa vitabu na majarida. Ameongeza kwamba wizara imeandaa kanzi data ili kuwatambua wataalamu wa kiswahili nchini katika ngazi zote.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Consolata Mushi amesema Kongamano hilo litasaidia kubadilishana uzoefu na kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowapata wanahabari katika kutumia Kiswahili katika kazi zao. Amesema uzinduzi wa Kamusi Kuu ya Kiswahili Toleo la 3 utaongeza ufanisi katika tasnia ya habari kwa idhaa zinazotumia lugha ya Kiswahili kutokana na uwepo wa maneno zaidi ya mia moja mapya.

Kongamano hilo la siku tano linabeba kauli mbiu isemayo Tasnia ya Habari kwa Maendeleo ya Kiswahili Duniani huku likishirikisha wadau wa Kiswahili na vyombo vya habari kutoka ndani na nje ya nchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi