Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Afanya Mazungumzo na Rais wa Ureno
Jun 30, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Ureno, Mhe. Marcelo Rebelo de Sousa, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu ya Ureno Mjini Lisbon.

Katika mazungumzo hayo viongozi hao wamejadili namna ya kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Ureno hususani katika sekta ya uchumi wa buluu kwa kutumia rasilimali za bahari kwa kuzingatia Ureno imepata maendeleo zaidi katika sekta hiyo.

Makamu wa Rais amemueleza Rais wa Ureno adhma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza uchumi wa buluu ikiwemo mikakati ya kutumia vema bahari na rasilimali zake. Amesema Tanzania imejaaliwa kuwa na ukanda mrefu wa Pwani wa takribani kilomita 1,450 na Ukanda wa Kiuchumi wa Kipekee unaofikia kilomita za mraba 223,000 hivyo ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili utakua na manufaa zaidi.

Pia, Makamu wa Rais amesema Tanzania imeweka mikakati ya kujenga bandari ya Uvuvi katika bahari ya Hindi pamoja na  ziwa Victoria na Tanganyika itakayochangia katika kuongeza mapato katika sekta hiyo.

Kwa upande wake Rais wa Ureno, Mhe. Marcelo Rebelo de Sousa amesema Ureno ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kujenga bandari ya uvuvi itakayosaidia Tanzania kunufaika zaidi kupitia rasilimali za bahari na kuimarisha uchumi wa buluu.

Halikadhalika Rais Marcelo ameongeza kwamba Ureno ipo tayari kushirikiana na kuhakikisha Tanzania inapiga hatua za kimaendeleo katika uchumi wa buluu pamoja na kukuza sekta ya biashara na uwekezaji.

Makamu wa Rais yupo nchini Ureno kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhifadhi wa Bahari na Rasilimali zake wenye lengo la kuhamasisha juhudi za Mataifa katika kufanikisha utekelezaji wa Lengo la 14 la Maendeleo Endelevu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi