Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 07 Septemba, 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA) ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia, Mheshimiwa Hailemariam Desalegn, mazungumzo yaliyofanyika kando ya ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kigali nchini Rwanda.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amemueleza Desalegn dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuinua sekta ya kilimo hususani kuongeza uzalishaji pamoja kuwavutia zaidi vijana na wanawake ambao ni idadi kubwa iliyopo kushiriki katika sekta hiyo. Amesema Serikali imeongeza bajeti katika sekta ya kilimo kutoka Shilingi bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Shilingi bilioni 751 mwaka 2022/2023 ambapo uzalishaji wa mbegu bora na uazishwaji wa skimu za umwagiliaji ukiendelea.
Aidha, amesema Serikali imeanzisha Program maalum iitwayo “Building Better Tomorrow” ambayo inawalenga wanawake na vijana kushiriki katika kilimo ambapo pamoja na mambo mengine imelenga kuanzisha miradi kilimo cha biashara kuanzia 12,000 katika vijiji 12,000 nchi nzima, hivyo ni muhimu jumuiya na taasisi zinazoendeleza kilimo ikiwemo AGRA kuunga mkono ajenda hiyo.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na ardhi pamoja na eneo zuri la kijiografia ambalo linaweza kutumika katika kuchangia usalama wa chakula barani Afrika, hivyo kuwakaribisha wawekezaji katika sekta ya kilimo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA) ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia, Mheshimiwa Hailemariam Desalegn amesema AGRA inaunga mkono jitihada za Tanzania katika kuinua sekta ya kilimo na ipo tayari kushirikiana na taasisi zingine katika ufadhili wa programu mbalimbali za miradi ya kilimo ikiwemo “Building Better Tomorrow”.
Aidha, ameongeza kwamba sekta ya kilimo barani Afrika inapaswa kuendana na maendeleo ya teknolojia kwa kuwekeza katika teknolojia rafiki ili kuweza kufanya kilimo cha kisasa, kufanya uzalishaji bora na baadae kuweza kuvutia vijana zaidi.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame, mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kigali nchini Rwanda. Mazungumzo hayo yamefanyika kabla ya kuanza kwa mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wanaoshiriki majadiliano katika mkutano wa Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika leo tarehe 7 Septemba 2022.
Pia Makamu wa Rais amefanya mazungumzo na Rais mteule wa Mfuko wa Ufadhili wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) Alvaro Lario, Mazungumzo yaliyofanyika kando ya ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kigali nchini Rwanda.
Mazungumzo hayo yamelenga kuongeza ushirikiano baina ya Tanzania na Mfuko huo kwa lengo la kuendeleza miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa lengo la kuendeleza sekta ya kilimo nchini Tanzania.