Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makampuni ya Uchimbaji Madini Yatakiwa Kutekeleza Mipango ya Kurekebisha Upya Maeneo ya Uchimbaji
Aug 12, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Makampuni ya uchimbaji wa madini nchini, yametakiwa kutekeleza mipango yao ya kurekebisha upya maeneo ya uchimbaji wa madini (rehabilitate and Renewal) badala ya kuacha mashimo peke yake ikiwa ni njia mojawapo ya kutunza mazingira.

 

Hayo yamezungumzwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango wakati akishiriki katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) yaliyofanyika leo Agosti 12, 2022 jijini Dodoma.

“Shughuli za uchimbaji wa madini hazizingatii shughuli za utunzaji wa mazingira, naiagiza Wizara ya Madini kuongeza kasi ya ukaguzi wa migodi mikubwa na midogo ili kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria wachimbaji wanaozembea na kuchafua mazingira ikiwemo kuacha mashimo baada ya kuisha kwa shughuli za uchimbaji”, alisema Dkt. Philip Mpango.

Vilevile, Makamu wa Rais amewataka Wizara ya Madini, Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) kushirikiana kuhakikisha Sheria na Kanuni za afya na usalama mahala pa kazi zinafuatwa na kuweka haraka utaratibu utakaowezesha kudhibiti changamoto ya kuongezeka kwa wagonjwa wanaoathirika na vumbi linalotokana na uchimbaji wa madini.

Amelitaka Shirika hilo kushirikiana na SIDO kuongeza jitihada za kubuni ikiwa ni pamoja na kutengeneza zana bora za uchimbaji wa madini zenye gharama nafuu kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Pia, kuimarisha mafunzo hasa kwa mafundi mchundo.

Kwa upande mwingine, Makamu wa Rais amelipongeza shirika hilo kwa kufanya mapinduzi makubwa ya kiutendaji kwa kuongeza ubunifu, kuimarisha uzalishaji na kujenga misingi mizuri ya kujiendesha kibiashara na kupunguza utegemezi wa moja kwa moja Serikalini kutoka asilimia 89% mwaka 2018/19 mpaka 13.2% mwaka 2021/2022 na kuliwezesha shirika hilo kutoa gawio la Shilingi bilioni 4.3 kwa mwaka wa fedha 2021/22.

“Nawapongeza pia kwa kujiongeza kubuni na kuanzisha miradi mipya ya kutengeneza nishati mbadala inayotokana na makaa ya mawe kwa ajili ya kupikia kwani nishati hii italeta mapinduzi makubwa katika sekta ya nishati nchini kwa kupunguza matumizi ya mbao, miti na kuni yatakayopunguza uharibifu wa mazingira”, alisema Dkt. Mpango.

Vilevile, Makamu wa Rais ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani ya madini kutoka katika hatua ya utafutaji, uchorongaji, uchimbaji, uchenjuaji, uongezaji wa thamani na biashara ya madini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi