Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Majaliwa Stadium Itakuwa ya Kisasa - Dkt.Mwakyembe
Aug 13, 2020
Na Msemaji Mkuu

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akigusa nyasi na kushuhudia hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa uwanja wa Majaliwa Stadium kutoka kwa viongozi wa Wilaya ya Ruangwa wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Bw. Hashim Mgadwila (Kaunda suti) mnamo Agosti 12,2020 alipotembelea uwanja huo.

Na Shamimu Nyaki –WHUSM, Ruangwa

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi kwa ujenzi wa uwanja wa Majaliwa Stadium ambao unajengwa kwa kuzingatia  viwango vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Dkt. Mwakyembe ametoa pongezi hizo Agosti 12, 2020 alipotembelea uwanja huo ambapo amesema kuwa eneo la kuchezea (pitch) lina nyasi bora ambazo zina viwango vinavyohitajika katika viwanja vya soka duniani.

“Uwanja huu utakapokamilika utakuwa ni uwanja wa kisasa kwa sababu ujenzi wake unazingatia viwango vya kimataifa ikiwemo vyumba bora vya kubadilishia nguo, maduka ya kuuza jezi mbalimbali, majukwaa ya hadhi tofauti hivyo naipongeza sana Halmshauri ya Ruangwa kwa uwekezaji huu”, alisema Dkt.Mwakyembe.

Aidha, Dkt. Mwakyembe ameishauri halmashauri hiyo kufikiria kuweka nyasi bandia katika uwanja huo kwa kuwa nyasi hizo zinatumia gharama nafuu katika utunzaji na zinasaidia shughuli mbalimbali kufanyika bila kuharibika tofauti na nyasi halisi.

Vilevile, Waziri Mwakyembe ameipongeza halmashauri hiyo kwa kuilea vizuri timu ya Namungo FC ambayo imefanya vizuri katika ligi kuu na mashindano ya Kombe la shirikisho hatua iliyoifanya timu hiyo kufuzu kuiwakilisha nchi katika Kombe la shirikisho barani Afrika.

Kwa upande wake Afisa Mipango wa Halmshauri hiyo, Bw. Fundikira Masamalo amesema kuwa uwanja huo utakua na majukwaa mbalimbali ikiwemo jukwaa kuu ambalo litakuwa na uwezo wa kubeba mashabiki takriban 1,200.

Uwanja huo unatarajiwa kuwa na viwango vinavyofanana na Uwanja wa Benjamin Mkapa wa Dar es Salaam na utatumika katika ligi mbalimbali na michezo mingine.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi