Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza kampuni zote zilizopewa kazi za upimaji wa viwanja kwenye Jiji la Dodoma na zimeshindwa kukamilisha kazi hiyo, ziwe zilikuwa na mikataba ama hazikuwa na mikataba zichukuliwe hatua kali za kisheria.
“Moja kati ya hatua hizo, ni kuziblacklist kwa sababu makampuni hayo yapo, tutumie makampuni ambayo yana uaminifu badala ya kutumia makampuni ambayo yanatuzalishia migogoro,” alisema.
Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma cha viongozi wa majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga na Dodoma ili kujadili migogoro ya ardhi iliyokithiri kwenye majiji hayo na kutafuta suluhisho.
“Tunatambua makampuni mengi hapa Dodoma ni ya watumishi wenyewe kama ambavyo imeelezwa kwenye ripoti. Mkurugenzi alikuwa na kampuni mbili, Mhasibu wake ana kampuni yake na wanazitumia kupima maeneo, kwa hiyo ni miradi yao.”
Aliwaagiza Wakuu wa Mikoa wahakikishe kuwa Kamishna Msaidizi wa Mkoa, Maafisa Mipango Miji wa Majiji, Halmashauri na Manispaa hawana sababu ya kuchukua watumishi wa muda kufanya kazi ya upimaji bali wafanye wao ili kuepusha mianya ya rushwa.
Pia aligiza watafutwe na kukamatwa vibarua ambao wanatembea na nyaraka za Serikali na kuuza viwanja kwa niaba ya maofisa wa Jiji. “Bw. Justin Albert, Freddy Mathias, Elias na Magige watafutwe, wachunguzwe na vyombo vya dola kuhusu nyaraka za Serikali walizonazo, na wazirejeshe nyaraka za Serikali wanazozitumia vibaya kwa kuendelea kuuza viwanja maeneo ya Jiji ya Ukanda wa Kijani, Mkonze, Ndachi, Chinyika, Ng’ong’ona na Mkalama.”
“Hawa ni vibarua, lakini wana ramani na wanavijua viwanja vyote. Wao wanachofanya ni kufanya mauzo halafu wanapeleka kwa watu wao pale Jiji na hati zinatoka. Kwa hiyo, watafutwe na wanyang’anywe zile nyaraka ili wasiendelee kuuza viwanja,” aliagiza.