Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Majaliwa Akagua Ujenzi wa Nyumba za Makazi ya Wananchi Walioridhia Kuhama katika Hifadhi ya Ngorongoro
Mar 13, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, imetenga sh. bilioni 1.2 kwa ajili ya awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa nyumba za wananchi watakaokubali kwa hiari kuhama katika hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo inahusisha nyumba 103 ambazo zipo katika hatua mbalimbal ambazo ujenzi wake ulianza Februari 28, 2022 na hadi kufikia Machi 12, 2022 ujenzi wake umefikia asilimia 78. Nyumba hizo zinajengwa katika kijiji cha Msomera wilayani Handeni, Tanga.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Machi 13, 2022) wakati akizungumza na wananchi katika kijiji cha Msomera kabla ya kukagua ujenzi wa nyumba hizo ambazo kati yake nyumba 53 zimepauliwa na hatua za umaliziaji zinaendelea, nyumba 42 zipo hatua ya boma na nyumba 8 zipo katika hatua za ujenzi wa msingi. 


Kadhalika, Mhe. Majaliwa amezitaka Wizara, Taasisi na Idara zote za Serikali zinazoshughulikia uhamaji wa hiari wa wakazi katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kukamilisha zoezi hilo kwa ufanisi.

Waziri Mkuu amesema kuwa wananchi hao waliokubali kuhama kwa hiari licha ya kupewa nyumba na eneo lenye ukubwa wa ekari tatu kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za ufugaji. Wananchi hao wanahama ili shughuli za uhifadhi ziendelee katika eneo hilo.

"Serikali itahakikisha haki zote za binadamu zinazingatiwa katika zoezi hilo la kuwahamisha kwa hiari wananchi wanaoishi kwenye hifadhi ya Ngorongoro kwenda katika maeneo mbalimbali watakayayoyachagua kikiwemo kijiji hicho cha Msomera, ambapo tayari Serikali imeshapima viwanja 2,500 na kutenga eneo la ekari 1,700 Kwa ajili ya kilimo na malisho”.

Hata hivyo Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa  Mkoa wa Tanga wakutane na viongozi wa kijiji na wananchi wa eneo hilo ili waendelee kuwaelimisha kuhusu zoezi hilo na umuhimu wake kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema kuwa eneo hilo wamekusudia liwe shamba darasa la ufugaji wa kisasa wenye tija kiuchumi ili kuwasaidia wafugaji nchini waweze kunufaika zaidi na ufugaji wanaoufanya tofauti na ilivyo sasa, hivyo amewaomba watoe ushirikiano kwa Serikali yao.

Naye, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi na wananchi wa Handeni wahakikishe wanasimamia vizuri mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kuepusha migogoro ya ardhi. “Maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za ufugaji yalindwe na yatumike kama ilivyokusudiwa.”

Kwa upande wao wakazi wa kijiji cha Msomera wamesema wapo tayari kuwapokea wakazi wa Ngorongoro watakaokubali kwa hiari kuhamia karika kijiji chao, pia wanashukuru kwa kuwa ujio wao utaenda sambamba na uboreshwaji wa miundombinu ya huduma mbalimbali za kijamii kama maji, afya na umeme.

Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mratibu wa Mradi, Prof. Wakuru Magigi alisema kuwa mradi huo umebuniwa kukidhi mahitaji ya kuwa mji wa kisasa wa wafugaji na huduma zote muhimu za kijamii na za wanyama kama majosho na maeneo ya minada zitajengwa na kwamba wananchi watakao hamia katika eneo hilo watakabidhiwa hati za umiliki wa ardhi ambazo zitawasaidia kupata fursa za kifedha.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi