Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Majaji Wakuu Watoa Rai Nchi Zinazohusika Kujiunga na SEACJF
Oct 29, 2023
Majaji Wakuu Watoa Rai Nchi Zinazohusika Kujiunga na SEACJF
Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika wakiwa katika majadiliano wakati wa Mkutano Mkuu wa Majaji Wakuu hao uliofanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 23 hadi Oktoba, 26, 2023.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika wameendelea kutoa rai kwa Majaji Wakuu ambao nchi zao zipo Kusini na Mashariki mwa Afrika kujiunga na jukwaa la Majaji Wakuu wa nchi hizo ili kwa pamoja kuongeza nguvu katika masuala ya maendeleo ya Mahakama za barani Afrika.

Jaji Mkuu wa Namibia na aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa hilo ambaye amemaliza muda wake, Mhe. Peter Shivute ametoa rai hiyo Oktoba 26, 2023 mara baada ya kumaliza Mkutano Mkuu wa Majaji Wakuu hao uliofanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 23 hadi Oktoba, 26, 2023.

"Hatujaridhika na idadi ya wanachama tulionao, jukwaa hili litakuwa bora kama Majaji Wakuu wa nchi zote zinazohusika watafanikiwa kujiunga, hivyo tunaendelea kuwakaribisha kujiunga kwa sababu ni vizuri kwetu sisi wote kama Mahakama za bara la Afrika kuwa na kiwango kimoja cha maendeleo katika Uhuru na kanuni zote zinazoathiri Mahakama. Mahakama zinapata faida kubwa kwa kuwa mwanachama wa jukwaa hili”, alisema Mhe. Shivute.

Akizungumzia kwa ujumla kuhusu mkutano huo, Mhe. Shivute amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga muda wake kuja kufungua mkutano huo pamoja na kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuandaa mkutano huo mkubwa huku akifurahishwa pia na mahudhurio ya Majaji Wakuu wanachama ambapo jumla ya Majaji Wakuu 15 kati ya 16 wamehudhuria mkutano huo ambapo imewasaidia kujadili masuala mengi kwa pamoja.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Kenya, Mhe. Martha Koome pamoja na kusisitiza Majaji Wakuu kuendelea kujiunga na jukwaa hilo ili kuwa na sauti ya pamoja, ameishukuru Tanzania kwa ukarimu waliouonesha kwao kwa kipindi waliokuwa hapo.  Aidha, amevutiwa na majadiliano yaliyojadiliwa kuhusu utatuzi wa migogoro katika Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika, matumizi ya teknolojia katika utoaji wa haki pamoja na uamuzi wa utatuzi wa migogoro katika maeneo yao ambazo ni mada muhimu katika uendeshaji wa Mahakama za nchi wanachama.

“Mkutano huu umetuwezesha kukaa pamoja na kujadili masuala mbalimbali, mfano katika matumizi ya teknolojia, tumeweza kuona Tanzania imefika mbali kwa kuingiza matumizi ya akili bandia hasa kwenye kutafsiri mashauri, hivyo imetuwezesha na sisi kufahamu zaidi matumizi ya teknolojia. Vile vile, tumeweza kuzungumzia changamoto zetu na  jinsi tunavyoweza kusaidia watu wetu kupata haki zao mapema kwani watu wa nchi zote wako sawa na mahitaji yao ni sawa, wote wanahitaji kupata haki kwa wakati.” Alimalizia Mhe. Martha.
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi