Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mageuzi Sekta ya Ujenzi Yachangia Ongezeko la Pato la Taifa
Jun 19, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_3799" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Tanzania,Dkt John Pombe Magufuli amezindua Rasmi ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa ya Kimataifa ambayo treni ya kisasa inayotumia umeme itaweza kusafiri kwa mwendokasi wa kilomita 160 kwa saa.Kulia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa.[/caption]

Na Benjamin Sawe.

Mageuzi makubwa yanayoendelea katika Sekta ya Ujenzi nchini Tanzania yamechangia ongezeko la pato la Taifa kutoka asilimia 7.8 mwaka 2010 hadi asilimia 12.7 mwaka 2015.

Ukuaji wa sekta hii unatokana na kuongezeka kwa shughuli za ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji ikiwemo barabara,reli na madaraja, viwanja vya ndege na majengo mbalimbali ya kibiashara.

Hata hivyo, mafanikio haya hayajaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa umasikini na kuongezeka kwa upatikanaji wa wa ajira zenye staha. Hivyo, juhudi kubwa inahitajika katika kufuatilia utekelezaji wa Sera na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17-2020/21).

Mafanikio ya utekelezaji wa Sera na Mpango huo utafanikisha azma ya Taifa la kuondoka katika umasikini na kufikia uchumi wa kipato cha kati na Viwanda ifikapo mwaka 2025.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema kwamba Serikali inaendelea kutekeleza Sera ya kuunganisha mikoa yote na nchi zote jirani kwa barabara za lami. Amesema, katika mwaka wa fedha 2016/2017 miradi ya barabara yenye jumla ya takriban kilometa 987 na madaraja makubwa mawili imekamilika.

Amebainisha miradi iliyokamilika kuwa ni pamoja na ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Namtumbo – Kilimasera – Matemanga - Tunduru (km 187.9); Tunduru – Nakapanya – Mangaka (km 137.3) na Mangaka – Mtambaswala (km 65.5) katika Ukanda wa Kusini.

Kwa upande wa Ukanda wa Kaskazini, Prof. Mbarawa ameitaja miradi iliyokamika kuwa ni ukarabati wa barabara ya Mkumbara – Same (km 96) na ujenzi wa barabara ya Dodoma – Babati (sehemu ya Dodoma – Mayamaya - km 43.65).

Aidha, kwa upande wa Ukanda wa Kati na Magharibi miradi iliyokamilika ni ujenzi wa barabara ya Mbeya – Lwanjilo – Chunya (km 72), barabara ya Mwigumbi – Maswa – Bariadi – Lamadi (sehemu ya Bariadi – Lamadi - km 71.8), barabara ya Nzega – Puge (km 58.8), barabara ya Sitalike – Mpanda (km 36.9), barabara ya Tabora – Urambo - Ndono (km 94) na barabara ya Kyaka – Bugene – Kasulo (sehemu ya Kyaka - Bugene (km 59.1).

Kwa upande wa Ukanda wa Mashariki, ujenzi wa barabara ya Bagamoyo – Msata (km 64) umekamilika kwa kiwango cha lami. Madaraja makubwa yaliyokamilika ni Daraja la Kilombero na Daraja la Ruvu Chini.

Prof. Mbarawa amesema, Serikali imeanza maandalizi ya Awamu ya Pili ya ujenzi wa miundombinu ya BRT itakayohusisha barabara za Kilwa, Kawawa na Chang’ombe zenye urefu wa kilometa 20.3 na ujenzi wa flyovers katika makutano ya Chang’ombe na Uhasibu chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Waziri Mbarawa ambaye anafuatatilia kwa karibu sana utekelezaji wa miradi hiyo amesema kuwa, tarehe 20 Machi, 2017 Serikali ilitiliana saini na Benki ya Dunia mkataba wa mkopo wa kugharamia mradi wa uboreshaji wa usafiri katika Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Urban Transport Improvement Project).

Amefafanua kwamba, Mradi huo utahusisha ujenzi wa barabara za juu (Interchange) kwenye makutano ya Ubungo, ujenzi wa Miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Tatu na Awamu ya Nne.

Awamu ya Tatu itahusisha barabara za Azikiwe, Bibi Titi, Uhuru na Nyerere zenye urefu wa kilometa 23.6 kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi Gongo la Mboto. Awamu ya Nne itahusisha barabara za Ali Hassan Mwinyi, Sam Nujoma na Bagamoyo kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi Tegeta.

Katika Hotuba yake aliyoitoa hivi karibuni Bungeni, Profesa Mbarawa amesema mradi wa ujenzi wa barabara za juu (flyovers) na maboresho ya makutano ya barabara katika jiji la Dar es Salaam unahusisha ujenzi wa barabara za juu (Flyover) katika makutano ya TAZARA na Ubungo.

Amefafanua kwamba, maboresho ya makutano ya Chang’ombe na Uhasibu yatajumuisha ujenzi wa barabara ya juu na miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya II (BRT Phase II). Maboresho mengine yatafanyika katika makutano ya Magomeni, Mwenge, Tabata, KAMATA, Uhasibu (Kurasini) na Morocco.

Kwa upande wa Mradi wa barabara ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) hadi Pugu (km 8.0), Prof. Mbarawa amesema, barabara hii itajengwa njia sita. Hata hivyo, ujenzi wa barabara hiyo umesitishwa ili kupisha mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya tatu utakaotekelezwa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.

Mradi wa barabara ya Kimara – Kibaha (km 25.7) unahusisha upanuzi wa barabara hii kuwa njia sita ikijumuisha upanuzi wa madaraja ya Kibamba, Kiluvya na Mpiji. Hadi Machi, 2017 taratibu za kumpata mhandisi Mshauri kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi huu zimesitishwa kwa kuwa utajumuishwa kwenye awamu ya pili ya mradi wa Dar es Salaam Maritime Gateway chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.

Kutokana na umuhimu wa Sekta ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi katika maendeleo ya Taifa, mara tu baada ya kuchaguliwa kuwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli aliagiza ujenzi wa barabara ya kutoka Mwenge hadi Moroco ambayo ilikuwa na msongamano mkubwa wa magari kuelekea katikati ya jiji.

Msongamano huo umekuwa ukiathiri malengo ya Wafanyakazi ambao walikuwa wakitumia muda mwingi wakiwa kwenye foleni na hivyo kupunguza muda wa kufanya kazi lakini pia uzalishaji na utoaji huduma za msingi kwa Taifa.

Hivi karibuni Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa barabara za juu (fly over) katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela eneo la Tazara unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 100 za Kitanzania na makutano ya barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam.

Aidha, Prof. Makame Mbarawa amepokea Kivuko cha MV Kazi ambacho kimejengwa na Kampuni ya Kizalendo ya M/S Songoro Marine Transport Boatyard ya Mwanza kilicho. Kivuko hicho kilichogharimu jumla ya Shilingi bilioni 7.3, ni moja ya ahadi ya Mheshimiwa Rais John Magufuli alizozitoa wakati wa Kampeni zake za Urais.

Aidha, uzinduzi wa daraja la Kigamboni ni moja ya mafanikio makubwa ambayo yanafanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayotekeleza Ilani yake ya Chama Tawala cha CCM.

Daraja hilo lenye urefu wa mita 680 linaunganisha upande wa Kurasini na Kigamboni wenye urefu wa Kilometa 2.5. limegharimu shilingi bilioni 250 za Kitanzania.

     

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi