Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mafunzo ya Kuongeza Ubora na Tija Endelevu Viwandani Yafunguliwa
Oct 02, 2017
Na Msemaji Mkuu

Taarifa kwa Umma

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) imeandaa mafunzo ya siku tano kwa ajili ya kuongeza ubora, tija na ufanisi viwandani. Mafunzo hayo yameanza kutolewa leo, Benjamin William Mkapa Special Economic Zone iliyopo Mabibo External, Dar es Salaam kwa washiriki 25 kutoka Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (Export Processing Zones Authority, EPZA); na viwanda vyenye leseni ya EPZA; Tanzania Tooku Garment Factory, Kamal Steel Ltd, Quality Pulse, Hyses EPZ Company and Soman Agro Limited.

Mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa KAIZEN awamu ya pili; ambao utatekelezwa katika mikoa 8 (Dar es Salaam, Morogoro, Arusha, Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro, Singida, na Dodoma kuanzia mwaka huu (2017) hadi 2020. Lengo la mafunzo haya ni kuwajengea washiriki uelewa na umahiri katika kuitumia dhana ya KAIZEN; ambayo ni mbinu ya kiuongozi inayolenga kuwashirikisha wafanyakazi ili kuongeza ubora, tija na ufanisi wa  uzalishaji kwa namna ambayo ni endelevu. Awamu ya kwanza ya mradi huu ilitekelezwa kuanzia mwaka 2013 hadi 2016 katika baadhi ya viwanda vilivyopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma; na kuonesha mafanikio makubwa.

 “Kutokana na matokeo yaliyopatikana na kuongezeka kwa tija katika viwanda vilivyofikiwa katika kipindi cha majaribio, sambamba na umuhimu wa tija katika maendeleo ya viwanda, Wizara imepanga kuweka mazingira yatakayowezesha kutumika kwa mfumo wa KAIZEN katika viwanda vyetu”, alidokeza mwakilishi kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Kwa kuzingatia umuhimu na uhitaji wa mfumo wa KAIZEN; Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji pamoja na JICA wamepanga kuwajengea uwezo washiriki wa mafunzo haya ili wawe wakufunzi wazalendo; ili baadaye waendelee kutoa mafunzo katika viwanda vilivyo chini ya EPZA.

EPZA imefarijika kuwa mwenyeji wa mafunzo haya na itatoa ushirikiano wa kutosha kwa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji pamoja na JICA katika kipindi chote cha mafunzo ya darasani na viwandani. Hii ni kutokana na nia ya Serikali kuchagiza uendelezaji wa viwanda nchini; kama ilivyoelekezwa katika Mpango wa Pili wa Kitaifa  wa Maendeleo wa Miaka Mitano (Second National Five Years Development Plan).

 “Tunafarijika kwamba mafunzo haya yataongeza ubora na uzalishaji wa bidhaa kutoka katika viwanda viivyopo nchini; na hivyo kuongeza ushindani wa nchi yetu wa kufanya bishara kimataifa na kuongeza uhitaji viwandani wa bidhaa na mali ghafi za ndani ya nchi.

Nyanda J. Shuli

Afisa Uhusiano kwa Umma Mkuu, EPZA.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi