Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mafanikio ya Ziara ya Rais Samia nchini India Yatajwa
Oct 12, 2023
Mafanikio ya Ziara ya Rais Samia nchini India Yatajwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bi. Zuhura Yunus akizungumza na Waandishi wa Habari leo Oktoba 12, 2023 kuhusu ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini India
Na Grace Semfuko, MAELEZO.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bi. Zuhura Yunus amesema, ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini India, imekuwa na mafanikio makubwa ambapo katika ziara hiyo jumla ya hati 15 za makubaliano zilisainiwa na kati ya hizo, hati kumi zilikuwa ni makubaliano baina ya Taasisi za Serikali za nchi hizo na hati tano zilikuwa ni baina ya Sekta Binafsi.

Amesema lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo, na hasa katika sekta za kimkakati ikiwepo Sekta ya Afya, Kilimo, Viwanda, Ulinzi na Usalama wa bahari pamoja na kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zilizopo nchini Tanzania.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Oktoba 12, 2023 kuhusu ziara hiyo, Bi. Yunus amesema hati zilizosainiwa zilikuwa ni makubaliano kwenye sekta ya afya na taasisi za afya za India, uimarishaji wa masuala ya kidigitali, ushirikiano wa masuala ya utamaduni, kongani za viwanda, ukarabati na ujenzi wa vyombo vya majini pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC kushirikiana na Taasisi ya India ya Uwekezaji.

Katika mkutano huo na Waandishi wa Habari uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mawaziri walioambatana na Mhe. Rais walizungumzia jinsi ambavyo Wizara zao zilivyonufaika na makubaliano hayo.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya Umy Mwalimu amesema katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani, zaidi ya Trilioni 6 zimewekezwa katika sekta ya afya, ambapo katika ziara yake nchini India pia Rais ameweza kushawishi na kurudi na mambo yenye tija ikiwepo kusaini hati tatu za makubaliano zikiwepo hati mbili za utoaji wa huduma za matibabu kati ya Serikali ya Tanzania pamoja na hospitali za BLK-Max na Rainbow inayoshughulikia masuala ya Watoto pekee huku hati ya tatu ikiwa ni ya makubaliano ya uzalishaji wa dawa na vifaa tiba.

“Suala la tiba mtandao ni sehemu ya makubaliano ambayo tumeingia kwamba tutabadilishana uzoefu kati ya wataalamu wa sekta ya afya wa India na Tanzania katika utoahi wa huduma za matibabu ya ubingwa bobezi, kwa hiyo wenzetu katika kutoa matibabu, suala la digital health au telemedicine ni sehemu ya utoaji wa huduma.” Amesema Ummy

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu kupatikana kwa soko la mbaazi nchini India amesema nchi hiyo ni mzalishaji na mtumiaji mkubwa wa bidhaa hiyo, hivyo kupatikana kwa soko hilo kumeiweka Tanzania kwenye ramani ya nchi ambazo ina makubaliano nazo ya kuuza zao hilo.

“India ni mtumiaji na mzalishaji mkubwa wa Mbaazi Duniani, kwa hiyo kupata uhakika wa kuuza bidhaa yetu kwenye soko lao ni jambo la msingi, kwa sababu kama hakuna makubaliano ya sisi na wao ,kwamba watatufungulia mlango wa kuuza mbaazi kwao, maana yake ni kwamba tunaishi bila kuwa na uhakika, kwa hiyo Tanzania inaingia kwenye ramani ya kwenye nchi ambazo tuna makubaliano nazo ambayo tutakuwa tunauza mbaazi kwao, ombi la Mhe. Rais ilikuwa ni angalau tupate robo ya tani laki tano lakini tani hizi laki mbili ndio angalau ni kiwango cha kawaida tulichokipata,” Amesema  Bashe.

Naye Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema ziara hii ya Mhe Rais kwa wizara yake imekuwa na mafanikio makubwa kwa sababu imekwenda kujibu changamoto za watanzania kuhusu upatikanaji wa rasilimali hiyo

“Ziara hii ya Mhe Rais sisi wizara ya Maji tulikuwa na ajenda ambayo aliibeba na kwenda nayo nchini India, kwamba ziwa Victoria, rasilimali ambayo ni toshelevu ni lazima itumike katika kutatua matatizo ya maji kwa watanzania, ukiangalia Jiji la Dodoma kabla Serikali haijahamia huko, mahitaji ya maji yalikuwa lita milioni 44, Mamlaka yetu ya maji ya DUWASA ilikuwa na uwezo wa kuzalisha lita Milioni 61, kwa hiyo Serikali ilipohamia Dodoma kumekuwa na ongezeko la watu, na mahitaji ya maji kwa sasa ni lita milioni 140, mahitaji ni makubwa kuliko uzalishaji wa mamlaka yetu ya maji, Mhe Rais akaona haja ya kuanzisha mradi mkubwa wa maji, kwa hiyo mradi huu utagharimu zaidi ya Dola milioni 600.”* Amesema  Aweso.

Kwa upande wake Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amesema lengo la kufanyika kwa Kongamano la Uwekezaji na Biashara wakati wa ziara ya Rais Samia nchini India ni kuhakikisha wafanyabiashara wa nchi hizo wanajadiliana na kuangalia fursa na vikwazo vya biashara na uwekezaji ili Serikali ziweze kuzifanyia kazi.

“Kulikuwepo na kongamano la uwekezaji na biashara nchini India, lilikuwa ni kati ya nchi yetu na India, kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na India, ili sasa, maana Serikali kwa Serikali tunaongea lakini hatufanyi biashara, ni wafanyabiashara ndio wanaofanya hizi takwimu za biashara na uwekezaji kuwa kubwa, kwa hiyo lazima muwawekee mazingira ya kuwasaidia na kuwaondolea vikwazo, hilo ndio lilikuwa ndio dhumuni kubwa la Kongamano lile, ”Amesema Makamba.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi