Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mafanikio ya Uwekezaji katika Miaka 60 ya Uhuru
Dec 09, 2021
Na Jacquiline Mrisho


-Kituo cha Uwekezaji chaanzishwa
-Maboresho ya Sera za kuvutia Uwekezaji
-Uwepo wa Wawekezaji wengi wa ndani na nje ya nchi.


Na Beatrice Sanga - MAELEZO


Baada ya Tanzania kupata Uhuru Mwaka 1961, Sera za Uwekezaji za Tanzania Bara zilihamasisha uwekezaji wa sekta binafsi, ikiwa ni ni pamoja na kutunga Sheria ya Kuhamasisha Uwekezaji wa Kutoka Nje ya nchi (Foreign Investment Protection Act), ya Mwaka 1963 hadi ilipofika mwaka 1967 ilipotangaza Azimio la Arusha ambapo Serikali ilisimamia na kuendesha shughuli kuu za uzalishaji, na kusababisha mvuto mdogo wa uwekezaji binafsi ikiwemo ule wa kutoka nje.


“Tunataka tuendelee kushughulika na umaskini wa watu wetu, tushughulike kwa dhati na matatizo ya wananchi ya uchumi wao, hali yao ya uchumi, hali yao ya viwandani, hali yao ya mashambani, hali yao ya shuleni, hali yao ya hospitalini.”


Ni moja ya kauli ya baba wa taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, juu ya serikali kuwekeza nguvu katika kutatua changamoto za wananchi ili kuondoa umaskini na kujenga taifa la watu huru kifikra na kiuchumi.


Hayati Mwalimu Nyerere aliamini kwamba ili uwe na taifa huru ni lazima watu wake wawe huru kiuchumi, kijamii, na kisiasa kuliko kutegemea misaada kutoka nchi zilizoendelea, na ndio maana alijikita katika kujenga jamii huru kwa kuanzisha ujenzi wa vijiji vya ujamaa, ili kuwaleta watanzania pamoja na kuweka msingi wa kushirikiana katika uzalishaji na uwekezaji.


Uwekezaji huu ulienda sambamba na ujenzi wa miundombinu, ili kurahisisha usafirishaji na usafiri wa bidhaa na watu kutoka sehemu moja hadi nyingine.


Baada ya kumaliza muda wake mwaka 1985 alipotangaza kung’atuka mwenyewe kutoka madarakani, Rais mwinyi alikamata usukani na kuanzisha sera za ushirikiano na mataifa ya nje katika uwekezaji ambapo ni wakati wa Mwinyi aliporuhusu biashara huria (Mzee wa Ruksa) ubinafsishaji na ushindani katika huduma za kijamii (Cost Sharing) ikiwa ni wakati ambao huduma zote ambazo zilikuwa zinatolewa bure wakati wa Hayati Nyerere zilianza kulipiwa na uwekezaji katika sekta mbalimbali uliongezeka.


Mwaka 1995 serikali ya Mkapa iliingia madarakani ambapo iliongozwa na sera ya ukweli na uwazi
Wakati alipohojiwa na Mwandishi wa kituo cha radio cha Deutsche Welle Petra Stein hayati Benjamin Mkapa wakati wa utawala wake kuhusu uwekezaji alisema, “Hatuna mpango maalum kwa wawekezaji kutoka Ujerumani, lakini kwa jumla kwa wawekezaji wote kutoka nje tumeandaa mazingira ambayo wenye nia wanaweza kuwekeza kwa faida yao lakini vile vile kwa maendeleo kwa nchi yetu.”


Aidha, Hayati Benjamini Mkapa alianzisha Sheria ya Uwekezaji kwa ajili ya Wawekezaji wa Ndani na wa Nje pamoja na kuanzisha Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambacho kinafanya kazi mpaka sasa.


Matokeo ya uwekezaji wa hayati Mkapa ni kwamba mapato yaliongezeka karibu mara tatu kutoka dola 612,587 mwaka 1995 na kufikia dola 1,796,862 miaka kumi baadae ya utawala wake.


Mwaka 2005 hayati Mkapa alikabidhi kijiti kwa Rais wa Awamu ya nne Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye alikuja na sera ya kilimo kwanza akiwa na lengo la kuhimiza uwekezaji katika Sekta ya Kilimo ikiwa kwa wakati huo watanzania asilimia 80 walikuwa wanategemea kilimo kwa uti wa mgongo wa taifa.


Sera hiyo ilihimiza Serikali kuwekeza katika kilimo cha kisasa ili kukuza soko la bidhaa za ndani kutokana na uzalishaji viwandani,
Sera hii ilienda sambamba na uimarishwaji kwa sekta zingine ikiwemo miundombinu, ambapo kulishuhudiwa kuongezeka kwa mtandao wa barabara nchi nzima, kuongeza upatikanaji wa umeme kwa kujengwa kwa mitambo ya Songas unaozalisha umeme wa gesi kutoka Mtwara hadi Dar es salaam.


Dr. Kikwete alijenga maeneo mengi na kukaribisha wawekezaji wa kigeni na wa ndani kwa wingi na kusababisha kukua kwa sekta mbalimbali.
Mwaka 2015 Hayati Dr. John Magufuli aliingia madarakani ambapo alijikita katika kukuza uchumi wa nchi kwa kuwekeza zaidi katika miundombinu wezeshi ya ukuaji uchumi na uwekezaji hapa nchini.


Siku zote hayati Dr. Magufuli aliamini kuwa Tanzania ni nchi tajiri, “Nchi hii ni tajiri, Tanzania ni tajiri ndugu zangu kwahiyo wala tusiogope kuyasema haya na kusimama imara katika kulinda rasilimali zetu.”


“Nchi yetu ni tajiri nataka niwaeleze ukweli, kilichokuwa kinatusumbua ni ufisadi na wizi kikipatikana hiki hakiendi kwa watu walengwa, lakini tulichofanya kulingana na mazingira yaliyotengenezwa mazuri na waliotutangulia awamu ya kwanza, awamu ya pili, awamu ya tatu, awamu ya nne sisi awamu ya tano tumetumia hayo mazingira kuyaboresha zaidi na ndiyo maana mnaona kila kitu kiinawezekana mpaka wale waliozoea kutunyonya wanashangaa” Alisema Rais Magufuli.


Kauli ya nchi yetu tajiri alisema mara kwa mara kuonesha ni jinsi gani rasimali za nchi zinaweza kutumiwa katika uwekezaji na uzalishaji mali na ukaleta tija kwa taifa.


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu ipate Uhuru mwaka 1961 kupitia Awamu ya Kwanza hadi ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Hassan Suluhu imefanya juhudi mbalimbali ili kukuza uwekezaji, maendeleo ya sekta binafsi, ushiriki wa wananchi kwenye shughuli za kiuchumi pamoja na miradi ya kimkakati na uwekezaji Shabaha kubwa ya uwekezaji imejikita katika kupiga vita umasikini, ujinga na maradhi.
Kupitia uwekezaji nchi yetu imeweza kukuza ajira zenye kipato kupanua wigo wa kodi, kukuza teknolojia na kuhamasisha matumizi ya rasilimali watu.


Tangu Tanzania ipate uhuru, Serikali imefanikiwa chukua hatua ya makusudi za kukuza uchumi wa Taifa na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wake kwa kuhamasisha uwekezaji na ushiriki wa wananchi katika uchumi. Kutokana na juhudi hizo, Serikali imepata mafanikio ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini, kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, utoaji wa mikopo kwa wajasiliamali, ujenzi wa miundombinu (umeme, reli, barabara, madaraja, n.k), utaoaji wa elimu kwa wajasiriamali, utoaji wa huduma za kijamii (afya, elimu, n.k) na ujenzi wa vituo vya uwezeshaji.


Katika taarifa ya mafanikio katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (UWEKEZAJI), Mhe. Geoffrey Mwambe hivi karibuni jijini Dododma alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua nyingine za kuandaa, kusimamia na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwemo Sheria, Kanuni na Maelekezo yote yanayohusu uwekezaji ili kuhakikisha kuwa vikwazo vyote katika uwekezaji vinatambulika na kuondolewa pamoja na kuwa na mazingira rafiki na sawa katika uwekezaji.


“Serikali itaendelea kujenga mazingira wezeshi ambayo yatasaidia wananchi na sekta binafsi kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa Taifa pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, kuimarisha miundombinu (barabara, reli, madaraja, umeme, viwanja vya ndege) ili kupunguza gharama za uzalishaji, kutengwa kwa maeneo ya biashara, kuongeza ushiriki wa watanzania katika miradi ya kimkakati na miradi mikubwa ya uwekezaji, kuboresha utoaji wa mikopo kwa kupunguza riba na masharti mengine, kutoa elimu kwa wajasiriamali na kudhamini mikopo kwa wajasiriamali.” Alisema Mhe. Mwambe

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi