Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mabaraza 281 ya Wafanyakazi Katika Wizara na Taasisi Yaundwa ili Kupunguza Migogoro Sehemu za Kazi
Mar 13, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Immaculate Makilika - MAELEZO

Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuhakikisha mazingira ya kazi na haki za wafanyakazi nchini yanasimamiwa ipasavyo kwa kuimarisha taasisi za kazi, kuboresha vyombo vya utoaji haki sehemu kazi.

Akizungumza leo jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita madarakani, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa. Joyce Ndalichako alisema kuwa katika Sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaani Mei Mosi ya mwaka 2021, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alielekeza taasisi za umma kuunda mabaraza ili kuimarisha majadiliano ya pamoja katika maeneo ya kazi.

“Katika kutekeleza maagizo hayo, Ofisi yetu imeratibu uundwaji wa Mabaraza 281 ya Wafanyakazi katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Serikali za Mitaa pamoja na kuwapatia elimu ya haki za msingi za wafanyakazi na namna bora ya kuimarisha mahusiano kati ya mwajiri na waajiriwa kupitia mabaraza hayo, na hivyo kupunguza migogoro isiyo ya lazima sehemu za kazi”, alisema Waziri Ndalichako.

Aliongeza kuwa, kuhusu utatuaji wa kero za wafanyakazi na kulinda haki zao, Serikali ya Awamu ya Sita imefanyia kazi hoja na maombi ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA) yaliyowasilishwa kwa niaba ya wafanyakazi katika maadhimisho ya Mei Mosi 2021 Jijini Mwanza.

Waziri Ndalichako alifafanua mambo hayo ikiwemo “Kupunguza kodi kwenye mishahara kwa asilimia moja (1%) kutoka 9% mpaka 8%, kuboresha maslahi ya watumishi kwa kuwapandisha vyeo na kulipa malimbikizo ya mishahara na madeni mengine, kupunguza gharama kwa wafanyakazi za kulipia matibabu ya watoto wao kwa kuongeza umri wa watoto wanaopaswa kunufaika na huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutoka miaka 18 hadi 21”

Aidha, alieleza mambo mengine ikiwemo kufuta tozo ya asilimia 6 iliyokuwa ikitozwa kwa ajili ya kulinda thamani ya mkopo unaotolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo na kufuta riba ya asilimia 10 iliyokuwa ikitozwa kwa wanufaika wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu waliokuwa wanachelewa kuanza kufanya marejesho ya mikopo yao.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi