Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mabadiliko ya Uchaguzi Mdogo
Jul 11, 2018
Na Msemaji Mkuu

NEC

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi kwenye kata mbili mpya na kuahirisha uchaguzi wa kata nyingine nne na hivyo  kufanya jumla ya kata zenye uchaguzi kuwa 77 badala ya 79 zilizotangazwa awali.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage imezitaja kata hizo mpya kuwa ni Kelamfua iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Rombo na Kata ya Kitaya iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Nanyamba.

“Kwa mujibu wa Kifungu cha 13 (1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika Kata ya Kelamfua iliyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo na Kata ya Kitaya iliyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Nanyamba,” alisema Jaji Kaijage.

Mwenyekiti huyo wa Tume amesema kwamba nafasi zote mbili za Udiwani zimetokana na kujiuzulu kwa madiwani waliokuwa wamechaguliwa awali.

“Kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Tume inatoa taarifa kwa umma kuhusu uwepowa Uchaguzi mdogo wa Madiwani katika Kata hizo ambapo uteuzi wa Wagombea Udiwani utafanyika tarehe 16 Julai, kampeni zitaanza tarehe 17 Julai mpaka 11 Agosti na siku ya kupiga kura ni tarehe 12 Agosti,” alisema.

Jaji Kaijage amevialika vyama vya siasa, wadau wote wa uchaguzi na wananchi kwa ujumla kushiriki uchaguzi huo kwa kuzingatia ratiba, sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, miongozo na maelekezo ya Tume wakati wa kipindi chote cha uchaguzi mdogo.

Katika hatua nyingine Jaji Kaijage ametangaza kuahirishwa kwa uteuzi wa wagombea kwenye kata tatu za Tindabuligi, Kisesa, Katumba na Mlimba.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 41(2) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Tume inaviarifu vyama vya siasa na wananchi wote kuwa uteuzi wa wagombea uliokuwa umepangwa kufanyika siku ya Jumamosi tarehe 14 Julai, 2018 kwa ajili ya uchaguzi mdogo katika kata za Tindabuligi na Kisesa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Kata ya Katumba iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo na Kata ya Mlimba katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero umeahirishwa. Tume itatangaza hapo baadae tarehe nyingine za uteuzi na uchaguzi katika kata hizo,” alisema.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi