Na Salum Vuai, WHUMK
MAANDALIZI ya matengenezo ya jengo la Beit Al Ajaib lililoko Forodhani mjini Zanzibar yameanza kufuatia ziara ya ujumbe kutoka Wizara ya Urithi na Utamaduni ya serikali ya Oman.
Ujumbe huo unaoongozwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Salum Mohammed Mahruki, uliwasili nchini jana Mei 11, na leo ulitembelea jengo hilo kujionea hali halisi ya uchakavu uliosababisha lisite kutumika kama kivutio cha utalii kwa zaidi ya miaka mitano sasa.
Msafara wa timu hiyo pia umemjumuisha mshauri mwelekezi ambaye ni mtaalamu wa uhifadhi majengo Dk. Enrico d’Errico, ambaye amekuja mahsusi kushauri njia bora ya kulitengeneza jengo hilo na mengine ya kihistoria nchini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyowashirikisha watendaji wakuu wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Urithi na Utamaduni ya Oman Salum Mohammed Mahruki, aliomba jengo hilo lisafishwe haraka, wakati wataalamu wakifanya tathmini ya kina ili kujua ukubwa wa kazi hiyo.
“Kwa namna tulivyoliona jengo hili, ni lazima kazi ya kulitengeneza ianze haraka iwezekanavyo, vyenginevyo tutazidi kuchelewa kwani tayari muda mwingi umepotea tangu lilipopata hitilafu,” alisisitiza.
Alifahamisha kuwa, sura ya Mji Mkongwe wa Zanzibar inaongezewa haiba na kuwepo kwa jengo hilo, ambalo kila mtalii anayefika anastaajabishwa na kuvutiwa na utaalamu pamoja na malighafi zilizotumika kulisimamisha tangu mwaka 1883.
Aliongeza kuwa, serikali ya Oman chini ya uongozi wa Sultan Qaboos bin Said, na kwa mahaba aliyonayo kwa Zanzibar na watu wake, imedhamiria kwa dhati kusaidia kwa asilimia 100 ujenzi wa jengo hilo na kulifanya liwe la kisasa zaidi bila kuathiri taswira yake ya kale.
Aliomba ushirikiano wanaoupata kutoka serikalini na wananchi wa Zanzibar uendelee ili kuifanya kazi hiyo iwe nyepesi ingawa inaonekana kuwa ngumu kutokana na sanaa ya ujenzi wake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe wa Zanzibar Issa Sariboko Makarani, mpango wa kulifanyia matengenezo jengo hilo umepata baraka zote kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambako Mji Mkongwe wa Zanzibar umeorodheshwa miongoni mwa miji ya urithi wa kimataifa.
Alisema ukaguzi wa jengo hilo na mengine matatu waliyoyatembelea, ni sehemu ya makubaliano ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ile ya Oman yaliyofikiwa mjini Muscat takriban wiki mbili zilizopita juu ya mpango wa kuyatengeneza majengo hayo.
Alieleza kuwa, matengenezo ya Beit El Ajaib yanahitaji utaalamu mkubwa, hivyo pande zote mbili zimekubaliana kuwa wakandarasi watakaopewa kazi hiyo ni wale wanaokidhi viwango vinavyohitajika, ambao huenda wakawa wengine kwa kila mmoja kupewa eneo lake.
“Tunatarajia matengenezo haya yatakapokamilika, jengo hili litakuwa na muonekano wa kisasa na mvuto wa ziada, ambao tunaamini litavutia watalii wengi zaidi kuliko wale waliokuwa wanakuja kabla,” alieleza Mkurugenzi huyo.
Ujumbe huo pia ulitembelea jengo la Makumbusho ya Kasri, Ngome Kongwe na iliyokuwa nyumba ya kulelea watoto yatima Forodhani ambayo yote yanakabiliwa na uchakavu mkubwa.
Hata hivyo, kwa sasa serikali inaifanyia matengenezo nyumba iliyokuwa ya kulelea watoto yatima, ili itumike kuhifadhi vitu na kumbukumbu zote zitakazohamishwa kutoka Beit El Ajaib kupisha matengenezo hayo.
Kwa mara ya kwanza, baadhi ya kuta za Beit El Ajaib ziliporomoka mwezi Disemba 2012, na baadae Novemba 2015, na tangu hapo serikali imelifunga kwa matumizi yoyote, hali inayochangia kukosa mapato kutokana na ziara za kitalii zilizokuwa zimezoeleka kuonekana pahala hapo.