Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Maafisa Ugani Dodoma Wakabidhiwa Pikipiki
Jun 09, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Ahmed Sagaff – MAELEZO

Serikali imekabidhi pikipiki 25 kwa Maafisa Kilimo wa Jiji la Dodoma ikiwa ni sehemu ya jitihada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika kuboresha hali za wakulima na kukuza sekta ya kilimo nchini.

Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Naibu Meya wa jiji hilo, Mhe. Emmanuel Chibago amesema hatua hiyo itawafanya maafisa ugani kuwafikia wananchi kwa wakati.

“Wakulima walikuwa hawafikiwi kwa wakati kwa sababu ya changamoto ya usafiri lakini leo hii Rais Samia kaliona hili na akaamua kutoa vifaa, kwahiyo pongezi kubwa tumpe Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa hiki alichokifanya,” ameeleza Mhe. Chibago.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika Jiji la Dodoma, Bi. Yustina Munishi amearifu kuwa lengo la Serikali kutoa vitendea kazi hivyo ni kuongeza mchango wa sekta ya kilimo kwa asilimia 10 kwenye pato la Taifa ifikapo mwaka 2030.

“Kitendo hiki kitaongeza huduma za ugani kwa wakulima wetu, kitaongeza mnyororo wa thamani wa mazao na vitawasaidia kuwapa elimu bora wakulima,” amehabarisha Bi. Munishi.

Naye, Afisa Kilimo wa Kata ya Msalato, Bi. Fatma Mohamedi ameishukuru Serikali kwa kuwapa pikipiki hizo ambazo zinaboresha mazingira yao ya kufanya kazi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi