Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Maafisa Maendeleo ya Jamii Lazima Twende na Kasi ya Rais Samia - Waziri Dkt. Gwajima
Nov 08, 2022
Na Jacquiline Mrisho


Na WMJJWM, Dodoma


Maafisa Maendeleo ya Jamii wametakiwa kujipanga kwenda na kasi ya Serikali ili kuchochea maendeleo ya jamii sambamba na sera, mikakati, sheria  na miongozo mbalimbali wakati Serikali ikiendelea kufanyia kazi changamoto za upungufu wa watumishi, mazingira ya kazi na sheria ya taaluma hiyo nyeti.


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa hao wa Sekretarieti za Mikoa na Wakuu wa Idara za Maendeleo ya Jamii wa Mamlaka za Serikali za Mitaa jijini Dodoma Novemba 08, 2022 alipokuwa akifungua Mkutano wa Mwaka wa kada hiyo.
Dkt. Gwajima amesema, Serikali ina matumaini makubwa na mchango wa kada hii na itahakikisha inafanya uwezeshaji Ili kwenda na kasi iliyokusudiwa. 


"Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan anatambua umuhimu wa sekta ya maendeleo ya Jamii katika kuiwezesha Jamii kushiriki kujiletea maendeleo kwa kutumia rasilimali walizonazo hivyo kuwa kitovu cha maendeleo na ndiyo maana amechukua hatua ya kuunda wizara mama ya sekta hii na mambo mengi mazuri yanakuja amesema Mhe. Dkt. Gwajima.


Akielezea umuhimu wa kada ya maendeleo ya jamii kwenye sekta zote amewapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya katika kuwezesha mapambano ya kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa watoto huku akirejea mpango kazi wa Taifa wa kupambana na ukatili huo kwamba Serikali inakamilisha ya utekelezaji wa miaka mitano iliyopita ili kuja na mpango mpya ambao utajibu mahitaji ya sasa kwenye mapambano haya.


Aidha, amewapongeza Maafisa hao kwa kushirikiana na wanajamii hasa waliojitolea kupambana na vitendo vya ukatili na kuwahamasisha wananchi kushiriki shughuli za kiuchumi kupitia kampeni ya kijamii inayojulikana kwa jina la SMAUJATA hali inayochangia wananchi kuwa na uelewa na kutofumbia macho vitendo vya ukatili.


Mhe. Dkt. Gwajima amewakumbusha Maafisa Maendeleo ya Jamii masuala yanayotekelezwa na Serikali na kwamba wakayasimamie ambayo ni majukwaa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, utekelezaji wa ahadi za nchi kupitia Jukwaa la kizazi chenye usawa ambapo Tanzania ni kinara wa eneo la haki na usawa wa kiuchumi, programu ya malezi na makuzi ya watoto kwa kutoa mafunzo ya malezi chanya kwa wazazi na walezi. 


Mengine ni pamoja na utekelezaji wa Ajenda ya Kitaifa ya kuwekeza katika afya na maendeleo kwa vijana balehe, programu jumuishi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto, usimamizi wa NGOs pamoja na uratibu wa machinga.


Wakati huo huo, Waziri Dkt. Gwajima amezindua mwongozo wa majadiliano wa mila na desturi.


Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,  Dkt. Zainab Chaula amewataka Maafisa hao kutimiza majukumu yao kulingana na mipango iliyowekwa na sheria zilizopo "Maafisa Maendeleo ya Jamii, muda wa kuambiana umepita kila mmoja asimame vema fanyeni kazi na Wadau. kila mnachopanga Mpange na Wadau", amesema Dkt. Chaula.


Mwakilishi wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI Naibu Katibu Mkuu, Ramadhami Kailima amebainisha kwamba, Maafisa Maendeleo ya Jamii ndio Wasimamizi na Watekelezaji na amewahimiza watumie Mikutano ya Mkoa na Wilaya kuzungumzia Majukumu yao.


Akizungumza katika kikao hicho,  Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la kutetea haki za wanawake na watoto la Kivulini, Yasin Ally amesema nchi haiwezi kufanikiwa bila kuwekeza kwenye Maendeleo ya Jamii.

Amewahimiza Maafisa Maendeleo ya Jamii kuthibitisha uwepo wao kwenye maeneo yao ambapo ameiomba Ofisi ya Rais - TAMISEMI kutoa Mwongozo wa Ulinzi na Usalama wa Mtoto na kuwepo Mpango kazi utaowezesha kukutana na Makundi Maalum.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi