Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Lindeni Mfuko kwa Kurejesha Mikopo- Msigwa
Oct 13, 2023
Lindeni Mfuko kwa Kurejesha Mikopo- Msigwa
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa akizungumza leo Oktoba 13, 2023 alipotembelea Ofisi za Mfuko wa Utamaduni na Sanaa
Na Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa ametoa rai kwa Wasanii kuwa mstari wa mbele kuulinda Mfuko wa Utamaduni na Sanaa kwa kufanya marejesho ya mikopo kwa wakati ili uweze kuendelea kuhudumia wengine.

Bw. Msigwa ameyasema hayo leo Oktoba 13, 2023 alipotembelea Ofisi za Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ambapo alipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya Wasanii ambao tayari wamenufaika na mikopo inayotolewa na Mfuko huo.

"Hizi fedha zinategemea mzunguko kwa hiyo unapochukua mkopo hakikisha unarejesha kwa wakati ili wengine wapate na kuufanya hai wakati wote", amesema Bw. Msigwa.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuinua Sekta ya Sanaa kwa kuwa ina umuhimu mkubwa sana kwa jamii hasa ikibadilishwa kuwa bidhaa inayoweza kurejesha utimamu wa mwili na akili kupitia burudani.

Amesema  sekta hiyo inaendana na mabadiliko ya teknolojia inayowalazimu Wasanii kuendelea kuhitaji huduma ya mikopo, hivyo  wana wajibu wa kuhakikisha wanaendelea kuthamini  juhudi za serikali kwa kuutunza Mfuko huo.

Kwa upande wao Wasanii walionufaika akiwemo Muhsin Awadhi (Dkt. Cheni) na Abdul Msanga wakizungumza kwa nyakati tofauti wameishukuru serikali kwa kuwathamini na kuanzisha mfuko huo ambao umewawezesha kupata mikopo kwa wakati na kufanya shughuli zao kwa ubora na thamani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi