Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Lazima Tutoke Kwenye Kilimo cha Kujikimu- Hasunga
Nov 12, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Mathias Canal-WK, Dar es salaam

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ambayo ni utekelezaji wa Mpango wa Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo Nchini (TASFIP) unaolenga kukuza kilimo kwa asilimia 6 kwa mwaka.

Kwa kuzingatia hatua hizo, Wizara ya Kilimo imekusudia kuleta mageuzi ya kilimo kutoka mtazamo uliopo wa kilimo cha kujikimu hadi kufikia uendeshaji wa kilimo kwa mfumo wa kibiashara.

Hayo yamebainishwa leo Tarehe 12 Novemba 2018 na Waziri wa kilimo Mhe Japhet Ngailonga Hasunga (Mb) wakati akifanya mahojiano na Televisheni ya Taifa (TBC 1) Mara baada ya kuapishwa kuongoza Wizara hiyo Ikulu Jijini Dar es salaam.

Mhe Hasunga ameyataja maeneo matatu ambayo yanahitaji utekelezaji wa haraka. Mosi, Utekelezaji wa adhma ya serikali kuendeleza kilimo kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kwa kusimamia thabiti nguzo ya programu hiyo ikiwemo Usimamizi endelevu wa matumizi ya maji na ardhi.

Alisema kuwa Lengo la ASDP II ni kuleta mageuzi katika  Sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji na tija, kilimo cha kibiashara, kuongeza pato kwa wakulima hivyo nilazima kuwekwa mkakati madhubuti wa utekelezaji ili kufikia nalengo yaliyokusudiwa.

Pili, Hasunga alisema kuwa atashirikiana na wataalamu wote Wizarani ili Kuongeza tija na faida kwenye mazao na kuendeleza kilimo cha biashara na kuongeza thamani ya mazao.

Vilevile, alisema kuwa serikali imekusudia Kuboresha mazingira wezeshi, uratibu, ufatiliaji na tathmini katika sekta ya kilimo hivyo wataalamu katika Wizara ya kilimo wanapaswa kuongeza kasi ya uwajibikaji ili kutimizi adhma hiyo.

Alisema Wizara ya kilimo itaweka mkakati madhubuti wa kuhakikisha kuwa bei ya Mazao inaimarika huku akisisitiza kuwa kwa ushirikiano na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji atahakikisha wakulima wanapata masoko ya mazao yao.

Jambo la tatu alilolieleza Waziri Hasunga kuhusu utendaji wake katika Wizara ya kilimo ni pamoja na kusimamia kwa weledi upatikanaji wa pembejeo za kilimo na ili ziweze kuwafikia wakulima kwa wakati kote mchini.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya kilimo Mhe Innocent Lugha Bashungwa alisema kuwa anatambua kuwa asilimia zaidi ya 70 ya wananchi wanajishughulisha na kilimo hivyo Wizara itaweka mkakati madhubuti kuhakikisha kuwa kilimo kina imarika na kuwa na tija kwa wakulima wote.

Aliongeza kuwa upotevu wa mazao baada ya mavuno ni suala linalohitaji kuzingatiwa kwa kiasi kikubwa ili kunusuru hasara inayowakumba wakulima.

Alisema, Changamoto hiyo inadumaza uzalishaji hivyo kufifisha ndoto ya kufikia uchumi wa viwanda kwa wakati kama ilivyokusudiwa. Licha ya changamoto hiyo, Tanzania imeendelea kuzalisha chakula kwa wingi kupita mahitaji yaliyopo.

Bashungwa alisisitiza kuwa Upotevu huo una uhusiano na uchumi wa viwanda kwani mazao yanayopotea au kuharibika yalipaswa kusindikwa lakini kwa kutokupelekwa kwake, yanaharibika kabla ya kumfikia mlaji hivyo kusababisha hasara kwa wakulima waliowekeza nguvu na rasilimali nyinginezo kwa muda mrefu.

Sambamba na hayo alisema kuwa Kitaasisi Serikali inalenga kuleta muafaka na mlingano kati ya kazi za Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji hasa kwenye kazi zinazohusu miundombinu ya uhifadhi na utawala, kupunguza upotevu wa mazao kwa kuongeza thamani na uchakataji wa mazao ya kilimo.

 
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi