Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

LATRA Watakiwa Kuhamia Dodoma
Jul 13, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Gabriel Migire amemtaka Mkurugenzi Mkuu mpya wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA. Habibu Saidi Suluo kuhakikisha wanahamia Dodoma.

Migire ameyasema hayo akiongea wakati wa makabidhiano ya Ofisi kati ya Uongozi uliomaliza muda na uongozi mpya jijini Dar es Salaam na kusema kuwa kuhamia kwao Dodoma kutarahisisha utendaji kwani kwa sasa wanapotakiwa Dodoma hulazimika kusafiri hali inayoongeza gharama za uendeshaji.

“Nikupongeze Mkurugenzi kwa kuaminiwa na kupewa nafasi ya kuongoza Mamlaka hii, nikuagize sasa uharakishe taratibu za kuhamia Dodoma sababu Serikali kuu iko Dodoma na unatambua kuwa maelekezo ya Serikali ni taasisi zote makao Makuu yanapaswa kuwa Dodoma’, amesema Katibu Mkuu Migire.

Katibu Mkuu Migire ametumia nafasi hiyo kumtaka Mkurugenzi huyo kuhakikisha anashirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kudhibiti ajali ambazo zimekuwa zikiongezeka kwenye mabasi na treni.

Aidha, Katibu Mkuu Migire amewataka LATRA kuongeza jitihada katika utoaji wa elimu wananchi na wadau ili waweze kutumia mfumo wa Tiketi Mtandao kwa urahisi kwani mfumo huo unasidia kuboresha huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA. Habibu Suluo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kwa nafasi hiyo na kumuhakikishia Katibu Mkuu Migire kuwa atazingatia taratibu, kanuni na miongozo katika uendeshaji wa Mamlaka hiyo. ameomba ushirikiano kwa watumishi wa LATRA kwa kufanya kazi kwa pamoja ili kufikia matarajio ya wananchi.

Mkurugenzi Mkuu, CPA Suluo amechukua fursa hiyo kuomba ushirikiano kwa menejimenti na watumishi ili kuwezesha Mamlaka hiyo kufanya vizuri kiutendaji.

Mkurugenzi Mkuu, CPA Habibu Suluo amechukua nafasi ya Gilliard Ngewe ambaye amemaliza muda wake.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi