Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

“Kuanzia sasa Visimbuzi Kuonesha Chaneli za Ndani Bure” Dkt. Abbasi
Aug 30, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na. Immaculate Makilika na Bushiri Matenda

Serikali imesema kuwa kuanzia sasa, visimbuzi vya Starmedia, Digtek, Continental na TING vitaanza kuonesha channeli zote za ndani bila kutoza gharama yoyote kwa mtazamaji.

Akizungumza na  waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi alisema kuwa serikali imefikia uamuzi huo baada ya visimbuzi vya AZAM, ZUKU na DSTV kuzuiwa  kuonesha chaneli za ndani kulingana na aina ya leseni zao.

Akifafanua kuhusu mazungumzo kati ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe na wadau pamoja na wamiliki wa  vituo mbalimbali vya televisheni  nchini yaliyofanyika mapema jana, Dkt. Abbasi alisema kuwa  kuanzia sasa chaneli zote za ndani zinapaswa kuonekana bila kutoza gharama yoyote kwa mtazamaji.

“Ningependa watanzania wafahamu kwamba kuanzia sasa visimbuzi vya TING, Starmedia, Continental na Digtek vitaonesha takribani chaneli 34 za ndani bure, ili kutoa fursa ya kila mwananchi kuwa na haki ya kupata taarifa” alisema Dkt. Abbasi

Aidha, alielezea kuwa wadau hao pamoja na wamiliki wa vituo vya televisheni wameonesha kuridhishwa na hatua hiyo ya kwa vile Serikali imetengeneza miundombinu itakayoruhusu chaneli zao kuonekana nchi nzima.

Dkt. Abbasi, alisisitiza kuwa “tayari nchi imeandaa mifumo ya kuhakikisha kwamba bila kutegemea kampuni za nje, au zilizosajiliwa nje ya nchi, tulishajenga mifumo ya ndani ya kusaidia kurusha matangazo nchi nzima”

Vilevile, aliwatoa hofu watazamaji kwa kusema kuwa kufikia septemba 5, mwaka huu visimbuzi vyote vitakuwa na chaneli zote za ndani bila kutoza gharama yoyote kwa mtazamaji.

Kuhusu baadhi ya wateja kulalamikia visimbuzi vya Starmedia, kutoonesha chaneli za ndani, Dkt. Abbasi alisema wameshaagizwa kuvifungua vyote na zoezi hilo litaendelea hadi Septemba 5 ambapo wataonekana nchi nzima.

Dkt. Abbasi, alisema visimbuzi vya AZAM, ZUKU na DSTV hao wataendelea kuonesha maudhui mengine lakini sio chaneli za ndani kama leseni zinavyowataka.

Kikao kati ya Waziri Mwakyembe na wadau  na wamiliki wa televisheni  nchini, kimefanyika kwa lengo la kuwa na majadiliano ya pamoja baina serikali na wadau hao ili kupata muafaka kuhusu kutooneshwa kwa chaneli za ndani katika visimbuzi vilivyokiuka masharti ya leseni zao.

Aidha, kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Injinia James Kilaba, pamoja na wataalamu wake.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi