Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kongamano la Mafuta na Gesi Nchini Lafunguliwa Rasmi
Sep 25, 2018
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_35655" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akitoa hotuba ya ufunguzi wa Kongamano la Mafuta na Gesi, jijini Dar es Salaam, Septemba 24, 2018. Alitoa hotuba hiyo kwa niaba ya Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani).[/caption]

Na Veronica Simba – DAR ES SALAAM

Kongamano la pili la wadau wa mafuta na gesi limefunguliwa rasmi jijini Dar es Salaam, leo Septemba 24, 2018, ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba alimwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kama Mgeni Rasmi, akiambatana na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, aliyemwakilisha Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani.

Akisoma hotuba ya ufunguzi kwa niaba ya Waziri Mkuu; Makamba aliwaeleza wajumbe wa Kongamano hilo kwamba ujumbe muhimu kutoka kwa Waziri Mkuu  ni kuwa Tanzania imefanya maandalizi makubwa kwa ajili ya kunufaika na sekta ya gesi pamoja na mafuta.

Akizungumza na waandishi wa habari, muda mfupi baada ya ufunguzi rasmi wa Kongamano hilo, Waziri Makamba aliwaeleza kuwa, miongoni mwa maandalizi ambayo Tanzania imefanya ni pamoja na mabadiliko ya Sheria ili kuwezesha Taifa kunufaika zaidi na rasilimali za mafuta na gesi.

“Tumejiandaa kitaasisi, kimipango na kimikakati. Mathalani, kuna Mpango Mkakati mkubwa wa matumizi ya gesi kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisisitiza.

[caption id="attachment_35656" align="aligncenter" width="750"] Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Mafuta na Gesi, wakifuatilia uwasilishwaji wa mada mbalimbali katika siku ya kwanza ya kongamano hilo jijini Dar es Salaam, Septemba 24, 2018.[/caption]

Akifafanua zaidi, Waziri Makamba alisema kuwa kuna mipango ya kuanzisha viwanda vya mbolea na viwanda vingine vya kemikali ambavyo vitatumia gesi.

“Kwahiyo tunaona kwamba mambo ni mazuri. Serikali imejiandaa na kwa bahati nzuri washiriki wa Kongamano ni wengi; kwahiyo ni wakati mzuri kwa nchi yetu kunufaika na tasnia hii.”

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mgalu akielezea matumizi ya gesi katika kuzalisha umeme nchini, alisema kuwa, kwa sasa, Serikali inatumia asilimia 50 ya gesi katika kuzalisha umeme ambao unafikia megawati 1500.

Alisema kuwa, matarajio ya Serikali ni kuzalisha megawati 5000 za umeme ifikapo mwaka 2020; hivyo ndiyo maana Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji.

[caption id="attachment_35657" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba akimwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (hayupo pichani), kutoa hotuba ya kuwakaribisha washiriki wakati wa ufunguzi rasmi wa Kongamano la Mafuta na Gesi, Septemba 24, 2018 jijini Dar es Salaam.[/caption]

Awali, akisoma hotuba ya ufunguzi rasmi wa Kongamano hilo, kwa niaba ya Waziri wa Nishati; Naibu Waziri Mgalu alieleza wapi Tanzania imetoka, ilipo na inakoelekea kwenye sekta ya gesi na mafuta.

Naye mwandaaji mkuu wa Kongamano hilo, Abdulsamad Abdulrahim, alitumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania kujitokeza kwa wingi na kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi nchini.

Zaidi ya Mataifa 75 kutoka nchi mbalimbali duniani, yamewakilishwa katika Kongamano hilo la siku mbili, linalotarajiwa kuhitimishwa kesho, Septemba 25, 2018.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi