Imeelezwa kuwa pindi Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma utakapokamilika utafungua usafiri wa anga kwa Mkoa wa Mara na kuwa kiunganishi kikubwa na mikoa jirani ya Kanda ya Ziwa.
Hayo yamesemwa mkoani Mara na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati akikagua ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami wenye urefu wa kilometa 1.75 ambapo utaruhusu ndege za Q400 Bombadier kutua kwa urahisi kiwanjani hapo.
Prof. Mbarawa amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 35.047 na mkandarasi anayetelekeza mradi huo ni Beijing Construction Company Limited ambapo kazi zinaendelea kwa kasi.
“Kiwanja cha Ndege cha Musoma kitakapokamilika kitafungua anga kwa kiasi kikubwa na kukuza uchumi wa mkoa wa Mara na mikoa jirani”, amesema Prof. Mbarawa.
Kuhusu suala la fidia, Waziri Mbarawa amesema Serikali imekwisha lipa fidia kiasi cha shilingi Bilioni 3.955 kwa wananchi waliopisha ujenzi huo.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma, Bw. Frank Msoffe amesema kuwa ujenzi wa kiwanja hicho utakapokamilika utatoka katika daraja la 2C na kwenda 3C na kuruhusu kupokea ndege zenye uwezo wa kubeba abiria 70 hadi 80.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe, ameeleza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba 2022 na unahusisha barabara ya kuruka na kutua ndege, barabara ya maegesho ya ndege, jengo la kuongezea ndege na jengo la zima moto.
Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Sanzate – Nata (km 40) kwa kiwango cha lami inayojengwa kwa gharama ya zaidi shilingi bilioni 39 na kumuagiza mkandarasi China Railway Seventh Group kuongeza kasi ya ujenzi huo na kukamamilisha kwa muda uliopangwa wa miezi 24.
Prof. Mbarawa amesema kiasi cha shilingi Bilioni 1.047 zitalipwa kwa ajili ya kulipa fidia wananchi 291 waliopiriwa na ujenzi wa barabara hiyo.
Barabara hiyo ni sehemu ya barabara kutoka Musoma – Arusha kupitia Serengeti Mto wa Mbu ambayo ni kiungo muhimu kati ya Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kaskazini na nchi jirani ya Kenya.
Waziri Mbarawa yupo mkoani Mara kwa ziara ya siku mbili ya kukagua utekelezaji wa miradi inayoendelea kutekelezwa na Wizara yake.