Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kupitia kampuni tanzu ya Mkulazi inayomilikiwa na Mfuko huo kwa asilimia 96 na Magereza kwa asilimia 4, wametoa jumla ya ajira 8,302 ndani ya miezi 15 tangu kilivyoanza uzalishaji mwezi Desemba 2023.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Bw. Masha Mshomba ametoa takwimu hizo leo Machi 17, 2025 katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mfuko huo ndani ya kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Bw. Mshomba amesema kuwa, ndani ya miezi 8 ya uzalishaji wa sukari ya majumbani, kumekuwa na mafanikio makubwa ambapo kufikia mwezi Februari 2025, jumla ya tani 19,124 za sukari ya majumbani zilikuwa zimezalishwa na kupelekwa sokoni huku lengo la kiwanda hicho ni kufikisha uzalishaji wa tani 50,000 ndani ya miaka mitatu.
“Kuanza uzalishaji wa sukari katika kiwanda cha Mkulazi kumesaidia kupunguza tatizo la uhaba wa sukari nchini na kuchangia kuongeza ajira kwa wananchi hivyo kupunguza umasikini kwani kiwanda hicho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kutoa ajira 11,315 huku ajira 2,315 zikiwa ni za moja kwa moja na 9,000 zisizo za moja kwa moja, kiwanda pia kimesaidia kukuza Mfuko”, alisema Bw. Mshomba.
Ameongeza kuwa, kutokana na manufaa ya kiwanda hicho, Rais alitoa maagizo ya kuangalia uwezekano wa kuwa na viwanda vingine kama hivyo, Mfuko unaendelea kufanyia kazi maagizo hayo.
Amefafanua kuwa, kwa jinsi kiwanda hicho kilivyotengenezwa, kinaweza kuzalisha sukari tani 75,000 kwa mwaka. Mradi huo pia unatarajiwa kuzalisha megawati 15 za umeme ambazo kati yake, megawati 7 zinatarajiwa kuingizwa katika gridi ya Taifa kupitia kituo cha kupokelea na kupoza umeme cha Msamvu Morogoro.
Ujenzi wa kiwanda hicho umekamilika mwezi Novemba 2023 na kuanza uzalishaji mwezi Desemba 2023. Kiwanda hicho kilizunduliwa tarehe 7 Agosti 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya uzalishaji wa sukari ya majumbani kuanza rasmi mwezi Julai 2024.