Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kivuko Kipya cha Mv. Chato II Kuboresha Usafiri Chato Nkome
Jan 05, 2021
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) imeendelea kuboresha huduma za usafiri wa majini nchini baada ya kupokea kivuko kipya cha MV.CHATO II HAPA KAZI TU ambacho ujenzi wake umekamilika. Kivuko hicho ambacho kimegharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.1 mpaka kukamilika kwake, kimejengwa na kampuni ya kizalendo ya Songoro Marine Transport Boatyard ya jijini Mwanza na kitakuwa kikitoa huduma kati ya Chato Muharamba na Nkome mkoani Geita.

Akizungumza wakati wa sherehe fupi ya kupokea kivuko hicho iliyofanyika mapema leo katika eneo la maegesho ya kivuko, maarufu kama ufukwe wa Chato mtaa wa Kalema Mkoani Geita, mgeni rasmi Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mheshimiwa Dkt. Leonard Chamuriho ameipongeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa kuweza kusimamia vyema ujenzi wa kivuko hicho hadi kukamilika kwake.

Aidha, ameitaka Wizara kuhakikisha inaendeleza utaratibu wa kujenga vivuko kwa kutumia wakandarasi wa ndani ambao unawawezesha kupata huduma kwa urahisi na kuongeza teknolojia na ajira kwa Watanzania.

Dkt. Chamuriho amesema ana Imani kuwa kupitia mradi huo wa ujenzi wa kivuko ambao umefanywa na kampuni ya kizalendo, Watanzania waliohusishwa katika ujenzi huo watakuwa wamejifunza teknolojia ya ujenzi wa vivuko na kwa kipato walichokipata wataweza kuboresha hali za maisha yao.

‘’Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa vivuko vyote nchini vinakuwa vya uhakika na salama kwa matumizi ya wananchi kwa kuendelea kuvifanyia matengenezo ya uhakika na kununua vipya pale vinapohitajika kadiri ya uwezo wa bajeti ya serikali unavyoruhusu’’. Alisema Dkt. Chamuriho.

Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuboresha usalama na usimamizi wa vivuko hivyo ili kuepusha matukio ya ajali kwa kuwaweka maafisa kutoka TASAC kusimamia maeneo yote yenye usafiri wa majini na kuendelea kutoa mafunzo kwa waendesha vyombo hivyo ikiwemo TEMESA ili kuwaongezea ufahamu juu ya kuzingatia taratibu na kanuni za uendeshaji wa vyombo vya majini.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle, akisoma taarifa fupi ya ujenzi wa kivuko hicho amesema kivuko cha MV.CHATO II kimejengwa kwa mfano wa meli (Landcraft) na sababu zilizopelekea kujengwa kwa mfumo huo ni katika kuzingatia mahitaji ya aina ya huduma itakayotolewa na kivuko hicho.

‘’Tunatarajia mizigo mingi itaongezeka kutoka na kuingia Chato kupitia Muharamba, Senga, Bukondo na Nkome, hivyo ujenzi wa kivuko hiki utakuwa ni chachu kubwa kwa wananchi wa Chato na maeneo ya jirani kuongeza na kukuza uchumi wao hasa kwa wenye kipato cha chini, aidha ni lengo la serikali kutoa usafiri wa uhakika na salama kwa wananchi popote panapohitajika’’, alisema Mhandisi Maselle

Vilevile, Mbunge wa jimbo la Chato ambaye pia ni Waziri wa Nishati Mheshimiwa Medard Kalemani akizungumza katika tukio hilo amesema anaishukuru serikali ya Awamu ya Tano kwa kufanikisha ujenzi wa kivuko hicho na kuongeza kuwa kivuko cha MV.CHATO II kitarahishisha shughuli za biashara kwa wafanyabiashara wa maeneo hayo kwani kitatoa fursa kwa wafanyabiashara hao kuweza kupeleka samaki na dagaa wao katika masoko ya Senda na Nchi jirani ya Congo DRC.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel akizungumza katika tukio hilo amesema ujenzi wa kivuko hicho ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi ambacho kilitoa ahadi ya kujenga kivuko kipya wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015. Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Dkt. John Magufuli kwa kuwezesha ujenzi wa kivuko hicho.

Kivuko cha MV. CHATO II HAPA KAZI TU, kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari madogo 10 sawa na tani 100 na kinafanya idadi ya vivuko hadi sasa kufikia 32 kote nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi