Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kituo cha Magufuli Kukamilika Juni 2022
Apr 27, 2022
Na Jacquiline Mrisho


Na Lilian Lundo - MAELEZO


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt.  Festo Dugange amesema kuwa kituo kikuu cha mabasi cha Magufuli kinatarajia kukamilika mwezi Juni mwaka huu ambapo kitaweza kutoa huduma kwa Wananchi kama ilivyokusudiwa.


Dkt. Dugange amesema hayo leo, Aprili 27, 2022 Bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kibamba, Mhe. Issa Jumanne ambapo aliuliza ni lini ujenzi wa kituo cha mabasi cha Magufuli utakamilika kwa asilimia 100 na Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kituo hiko kinafanya kazi kama ilivyokusudiwa.


“Hadi mwezi Machi, 2022 kiasi cha Shilingi bilioni 53.9 sawa na asilimia 94.5 zilikuwa zimelipwa kukamilisha ujenzi. Aidha, tarehe 14 Machi, 2022 Serikali imetoa msamaha wa kodi na sasa mkandarasi anaendelea na manunuzi ya vifaa ili kazi ya ujenzi iendelee na kukamilika mwezi Juni, 2022,” alifafanua Dkt. Dugange.


Aliendelea kusema kuwa, ujenzi wa kituo hicho ulianza Januari, 2019 kwa mkataba wa miezi 18 hivyo ujenzi ulipaswa kukamilika Julai, 2020. Aidha, Mkandarasi wa mradi huo aliongezewa muda wa ujenzi hadi Juni, 2022 kutokana na kuchelewa kutolewa kwa msamaha wa kodi wa vifaa vya ukamilishaji wa ujenzi huo.


Aidha, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Juliana Shonza, kuhusu lini serikali itaanza ujenzi wa stendi  kuu ya mkoa huo, Dkt.  Dugange  amesema kuwa, mkoa huo ni mkoa mpya na Serikali imeshaweka mpango wa kujenga stendi ya mabasi ya mkoa huo na tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya kujenga stendi ya kisasa mkoani humo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi