Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kikao cha FINA na Tanzania Chazaa Matunda katika Mchezo wa Kuogelea Nchini
Mar 15, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na John Mapepele - WUSM-

Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Duniani leo Machi 15, 2022 limeridhia kutoa ufadhili wa kuboresha miundombinu mbalimbali ya mchezo wa kuogelea hapa nchini, masomo na mafunzo ya mchezo wa kuogelea kwa vijana wa kitanzania pamoja na  kujenga bwawa kubwa la kuogelea lenye  viwango vya kimataifa vya Olimpiki ili kuweza kuisaidia Tanzania kupiga hatua  kwenye  mchezo huo katika anga za kimataifa.

Kauli hiyo imeitolewa Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Duniani (FINA), Bw. Husain AL Musallam baada ya kufanya mazungumzo na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa mjini Zanzibar, ambapo amesema FINA itaendelea kushirikiana na Chama cha Mchezo wa Kuogelea Tanzania (TSA) ili kuendeleza vipaji vya mchezo huo.

Katika mazungumzo hayo, Rais Husain AL Musallam, amefurahishwa na amepongeza juhudi na mikakati kabambe inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha  michezo, ambapo amesema amefurahishwa na mipango iliyopo ya kuendeleza miundombinu ya mchezo huo baada ya kutembelea na kuona eneo litakalojengwa miundombinu  kwa ajili ya mchezo huo unaojumuisha  Mpango Mkuu (Master Plan).

Mhe. Mchengerwa amemshukuru Rais Al Musallam  kwa ufadhili huo na kumweleza kuwa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imekusudia kuleta mapinduzi makubwa katika michezo na kwamba  tayari imeshatenga maeneo mbalimbali kwa ajili ya uwekezaji wa miundombinu ya mchezo huo ikiwa ni pamoja na mabwawa ya kuogelea yenye viwango vya Olimpiki.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Waziri alifuatana na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo.  Yusuph Singo ambapo baada ya mazungumzo hayo amemwelekeza kuhakikisha Idara ya Michezo inasimamia kwa ukaribu na ufanisi mchakato mzima wa kuwapata vijana watakaopelekwa masomoni kupitia ufadhili huo kwa  haki na kuwapata vijana wenye sifa, uwezo na kiu ya kufanya vizuri katika mchezo wa kuogelea ili kuinua kiwango cha mchezo huo hapa nchini.

“Tanzania ina vijana wenye vipaji na vipawa vya kufanya vizuri katika mchezo huu na kuliletea taifa heshima hivyo, nakuagiza uende ukasimamie kwa haki mchakato mzima wa kuwapata vijana wenye sifa bila upendeleo”. Amesisitiza Mhe, Mchengerwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi