Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Katibu Mkuu TAMISEMI Ataka Watumishi Korogwe Kubadilika Kiutendaji
Jul 06, 2017
Na Msemaji Mkuu

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Mussa Iyombe akizungumza na Watumishi wa Halmashauri za Mji na Wilaya ya Korogwe wakati wa ziara aliyoifanya wilayani Korogwe kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Umma katika kuwatumikia wananchi. Kulia kwake ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Bi. Zena Said na kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Robert Gabriel Ruhumbi.

Na. Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhandisi Mussa Iyombe, amewataka watumishi wa Halmashauri za Mji na Wilaya ya Korogwe kubadilika na kuboresha utendaji kazi wao kwa kutoa huduma bora kwa wananchi.

Katibu Mkuu Iyombe alitoa agizo hilo wakati wa kikao kazi alichokifanya katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe wakati wa ziara maalum ya kutembelea Halmashauri ya Mji wa Korogwe na Halmashauri zake ili kujionea utendaji kazi  na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi.

Katika kikao hicho Katibu Mkuu  Iyombe amepokea taarifa kutoka kwa Wakuu wa Idara  mbalimbali za  halmashauri za Mji na Wilaya  na pia alitumia nafasi hiyo kutoa maagizo  maalumu kwa watendaji hao ya kuwataka wabadilike na kuboresha utendaji wao sambamba na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Tawala (CCM) inayosisitiza juu ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhandisi Mussa Iyombe, akitoa maelekezo kwa viongozi wa Halmashauri za Mji na Wilaya ya Korogwe alipofanya ziara kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri hizo.

Aliwataka watumishi wanapotekeleza majukumu yao kukumbuka kuwa wao ni watumishi wa wananchi na ni wajibu wao kila wakati kuhakikisha wanawatumikia vema wananchi.

Aidha, aliwataka watumishi hao kujipima na kuona kama wanawahudumia wanachi inavyopaswa na pale ambapo hawafanyi vema ni jukumu lao kurekebisha hali hiyo ili wananchi waweze kupata huduma stahiki.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhandisi Mussa Iyombe, akipokea maelezo ya ujenzi wa shule ya Msingi Matondoro kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Robert Gabriel Ruhumbi (kulia). Shule hiyo imejengwa kwa ushirikiano wa wananchi na Halmashauri ya Mji wa Korogwe.

Katibu Mkuu huyo pia alitembelea baadhi ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na kuwaagiza watumishi hao kuwahimiza wananchi kuendelea kujitolea na kushiriki katika kujiletea maendeleo yao kwa kuchangia nguvu kazi na mali.

Kikao kazi hicho kilihudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Bi. Zena Said, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Robert Gabriel Ruhumbi, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe Mhe. Hilary Ngonyani pamoja na Watumishi wa Halmashauri za Mji wa Korogwe na Halmashauri ya Mji wa Korogwe.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi