[caption id="attachment_8737" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje Dkt.Aziz Mlima akizungumza na waandishi wa Habari hawapo pichani, kuhusu ujio wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere Convention Center Jijiji Dar es Salaam.[/caption]
Na: Thobias Robert- MAELEZO
Katibu Mkuu Jumuiya ya Madola Mh. Patricia Scotland anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku tatu hapa nchini.
Hayo yameelezwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Aziz Mlima wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Kituo cha Mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu huyo wa Jumuiya ya Madola atafanya ziara ya siku tatu nchini kuanzia Agosti 10 hadi 12 mwaka huu, ambapo atakutana na viongozi wa juu wa serikali ya Tanzania.
“Lengo la ziara hiyo nchini ni kuelezea viongozi wa ngazi za juu wa Tanzania kuhusu mageuzi yanayofanywa na Sekrtarieti ya Jumuiya ya Madola na vipaumbele vya Jumuiya hiyo kwa sasa, hatua zinazochukuliwa ili kuimarisha kazi za Jumuiya hiyo na kutoa taarifa kuhusu Mkutano wa Wakuu wa Nchi na serikali wa Jumuiya unaotarajiwa kufanyika jijini London nchini Uingereza mwakani mwezi April” alisema Dkt. Mlima.
Alifafanua kuwa mageuzi yanayotarajiwa kufanywa na Jumuiya hiyo ni pamoja na kuondoa vyeo vya Naibu Makatibu wakuu watatu na kupunguza idadi ya Wakurugenzi kutoka 12 hadi 6, kuanzisha nafasi tano za Maafisa Waandamizi kutoka maeneo ya kijiografia ya Jumuiya hiyo kwa maana ya Afrika, Ulaya, Amerika, Karibeani, Asia na Pacific Kusini kwa lengo la kuziba nafasi ya Makatibu Wakuu.
“Mageuzi haya yataiwezesha Jumuiya ya Madola kuokoa kiasi cha Pauni milioni 3 kwa mwaka ambazo zitafanya kazi mbalimbali za kimaendeleo kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo,” alifafanua Dkt. Mlima.
Katika ziara yake nchini, Katibu Mkuu huyo wa Jumuiya ya Madola anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mbali na kukutana na Rais Magufuli, Katibu Mkuu Scotland atafanya mazungumzo na Waziri wa Elimu, Sayansi, na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba.
Jumuiya ya Madola ilianzishwa karne ya 20 kwa lengo la kuikutanisha Uingereza na yaliyokuwa makoloni yake duniani kwa jukumu la kuhakikisha wanachama wanajikwamua katika nyanja za Kisiasa, Kiuchumi, kijamii, Michezo na Burudani huku Malkia wa Uingereza ndiye Kiongozi Mkuu wa Jumuiya hiyo.
Mpaka sasa Jumuiya hiyo ina nchi wanachama 53, huku Tanzania ikiwa ni moja ya wanachama ambapo imeshika nyadhifa mbalimbali, kwa kipindi cha mwaka 2013 hadi 2015 Tanzania ilikuwa Mwenyekiti wa kundi la Mawaziri la Utekelezaji la Jumuiya ya Madola likiwa na jukumu la kusimamia misingi mikuu ya Jumuiya hiyo.
Aidha, Tanzania ni mjumbe katika Bunge la Jumuiya ya Madola (CPA) ambapo mwaka 2007 hadi 2014 Marehemu Dkt. William F. Shija aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Bunge hilo.
Hivi karibuni katika kikao cha Maspika wa Bunge la Jumuiya ya Madola Afrika kilichofanyika mjini Abuja nchini Nigeria, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Maspika na kuwa Spika wa kwanza kutoka Tanzania kupata nafasi hiyo.