Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Karagwe Wapata Shule Mpya Kupitia Mradi wa Boost
Aug 04, 2023
Karagwe Wapata Shule Mpya Kupitia Mradi wa Boost
Muonekano wa shule mpya ya Awali na Msingi Nyakahita iliyopo Kata ya Kanoni, Wilaya Karagwe Mkoa wa Kagera.
Na Lucy Binamungu - Kagera

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma Mwassa amekagua ujenzi wa vyumba 16, jengo la utawala na matundu 18 ya vyoo katika shule mpya ya Awali na Msingi Nyakahita iliyopo Kata ya Kanoni, Wilaya Karagwe Mkoa wa Kagera.

Akizungumza na wananchi wa kata hiyo mara baada ya kukagua ujenzi wa shule, amewataka wananchi waendelee kumtumia Mbunge ambaye pia ni Waziri Wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Innocent Bashungwa katika kuwaletea maendeleo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye dira yake ni kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapata elimu bure

"Nafurahi kuona leo tunaweza kuwa na madarasa mazuri kwa sababu mwanafunzi wa chekechea kutembea umbali wa kilometa 8 kwenda na kurudi sawa na kilometa 16 sio suala la kawaida kwa mtoto. Sasa Serikali imewasikia  kinachobaki ni kuhakikisha watoto wote katika kijiji hiki wanapata haki yao ya kusoma na kuzifikia ndoto zao,” ameeleza Mhe. Mwassa

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Mhe. Julius Laizer ameeleza kuwa kutokana na wananchi wa kijiji hicho kuwa na uhitaji wa shule mara baada ya kupokea fedha kutoka Serikalini, walijitoa kushiriki katika ujenzi wa shule hiyo kwa kuchimba msingi, kusafisha eneo na kufanya kazi usiku na mchana ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati.

Ndg. Novath Ndibalema mmoja wa mwananchi wa Kijiji Cha Nyakahita amesema kuwa kabla ya ujenzi huo, wananchi waliamua kujenga vyumba vya udongo ili kuwanusuru watoto wadogo ambao walitembea umbali mrefu kwenda shule mama.

Wanafunzi hao walilazimika kuamka saa 10.30 alfajiri ili kuwahi masomo hivyo ukamilishaji wa shule hiyo na usajili wa wanafunzi utarahisisha mwendo kwa watoto wao na kupunguza wasiwasi ambapo watakaosajiliwa katika shule hiyo wanaotoka mbali hawatazidi kilomita moja.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Nyakahita, Mtungi Tirutangwa ameeleza kuwa shule mama ina wafunzi 1,765 kuanzia darasa la nne hadi la saba na shule shikizi ina wanafunzi 218 kuanzia chekechea hadi darasa la tatu huku ufaulu wa shule hiyo ni asilimia 60, hivyo anaamini uwepo wa shule mpya utaongeza ufaulu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi